CARCAS,Venezuela
RAIS wa Venezula Nicolás Maduro, amenusurika kuuawa baada ya kushambuliwa na ndege isiyokuwa na rubani alipokuwa akihutubia wakati wa kuadhimisha miaka 81 ya jeshi la nchi hiyo.
Tukio hilo lilitokea Caracas jana na katika picha za video Rais Maduro anaonyeshwa akitazama juu ghafla kwa hofu huku wanajeshi kadhaa wakikimbia.
Rais Maduro ambaye alishinda uchaguzi ulioghubikwa na utata, ameilaumu Colombia kwa shambulio hilo madai ambayo nchi hiyo imeyakanusha.
Taarifa zilisema katika tukio hilo wanajeshi saba walijeruhiwa na watu kadhaa walikamatwa.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mawasiliano, Jorge Rodriguez, ndege mbili zisizokuwa na rubani zililipua mabomu karibu na jukwaa la rais.
Rais Maduro baadaye alisema kuwa Kifaa kilichokuwa kinaruka kililipuka karibu yangu na sekunde chache baadaye ukatokea mlipuko wa pili.
Picha kwenye mitandao wa jamii zilionyesha walinzi wakimlinda Maduro wakitumia vifaa visivyopenya risasi baada ya shambulio hilo.