22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

RAIS WA PARAGUAY ANAPORUDISHA UDIKTETA KINYEMELA

UNAWEZA kusamehewa ukifikiri kuwa katika karne hii ya 21 demokrasia inayopigiwa upatu inatamalaki duniani kote, kwani hata baadhi ya viongozi wanaobinya demokrasia wanafanya hivyo kwa mbinu ili waonekane wanaiheshimu. Bado kuna viongozi duniani wenye mawazo mgando wanaoutamani udikteta kama ilivyodhihirika hivi karibuni nchini Paraguay wananchi wenye hasira walipochoma moto jengo la Bunge, wakipinga hila za Rais Horacio Manuel Cartes Jara kubuni njama ili kuurudisha udikteta kinyemela kupitia Seneti ya nchi hiyo iliyopiga kura kwa siri kumuidhinisha kugombea tena muhula mwingine kinyume na Katiba ya nchi hiyo.

 

Kiini cha utata huo ni ‘Rais mtata’ Cartes kutoka chama cha Colorado, mfanyabiashara mbobevu wa tumbaku, vinywaji na nyama aliyeingia madarakani miaka minne iliyopita. Amewahi pia kuwa Rais wa timu ya kandanda ya Libertad na timu ya Taifa tangu mwaka 2001 hadi 2012, hivyo hakuna shaka kuhusu uwezo wake kwenye biashara aliyoanza kujihusisha nayo tangu akiwa na miaka 19 kwenye kampuni ya kuunda ndege ndogo aina ya Cessna iliyomilikiwa na baba yake.

 

Lakini uwezo wake kisiasa unatia shaka ukizingatia rekodi yake ya uadilifu kabla hajawa Rais, mwaka 1986 alifungwa jela kwa siku 60 akituhumiwa kutakatisha fedha na mwaka 1989 alihukumiwa kifungo cha miaka saba kwa tuhuma kama hizo ingawa baadaye mwaka 2000 mahakama ilimfutia hatia. Polisi waliwahi kukamata ndege iliyojaa mihadarati katika shamba lake akakana kuhusika, akajitetea kuwa eti ndege hiyo ilitua kwa dharura kuepuka ajali lakini pia anatuhumiwa kimataifa kujihusisha na utakatishaji fedha.

 

Hakuwahi kuwa mwanasiasa hadi mwaka 2009 alipojitosa na kupuuzia shutuma dhidi ya chama alichojiunga (Colorado) kilichowahi kumuunga mkono dikteta mkatili, Alfredo Stroessner, aliyeitawala nchi hiyo kwa miaka 35 hadi mwaka 1989. Alijigamba kutohusika na mihadarati ndiyo maana aligombea urais mwaka 2013 na kushinda kwa asilimia 45.8 kwa kunadi sera za uhuru zaidi kwa sekta binafsi, kuboresha sekta ya umma na kuvutia wawekezaji wa kimataifa ikiwa ni mara ya pili tu katika miaka 202 ya uhuru wa taifa hilo chama tawala kukubali kukabidhi madaraka kwa upinzani ulioshinda.

 

Sekeseke lililoibuka Paraguay lililosababisha kuchomwa jengo la Bunge katika makabiliano baina ya waandamanaji na polisi na kusababisha kifo cha mwandamanaji Rodrigo Quintana, aliyepigwa risasi ya mpira kichwani limesababishwa na njama za Rais Cartes kujaribu kufuta kinyemela kipengele cha Katiba ya mwaka 1992 kinachomzuia Rais kugombea zaidi ya muhula mmoja.

 

Upinzani unaoongozwa na chama cha Liberal unapinga njama za ‘Mapinduzi’ baridi yaliyofanywa na Maseneta 25 kati ya 30 waliopiga kura kwa siri kupitisha Muswada wa Mabadiliko ya Katiba, ingawa mabadiliko hayo yanatakiwa kuridhiwa na kitengo kingine cha Bunge chenye wawakilishi wengi kutoka chama cha Rais Cartes.

 

Kinachowakasirisha wananchi wa Paraguay ni njama za kurudisha udikteta uliowatesa kwa miaka mingi wakikumbuka jinsi utawala wa kijeshi wa Jenerali Alfredo ulivyowakandamiza, hadi dikteta huyo alipong’olewa madarakani kwa Mapinduzi miezi sita tu katika muhula wake wa nane kwa mkakati uliosukwa na msaidizi wake Andrés Rodríguez, ili kumzuia asirithishe madaraka kwa mmojawapo kati ya wanawe wawili wenye sifa ya utumiaji mihadarati na ushoga.

 

Baada ya kupinduliwa Stroessner alikimbilia Brazil alikoishi kwa miaka 17 na ushei na kufariki dunia kutokana na kiharusi mwaka 2006 akiwa na umri wa miaka 93. Ili kufuta udikteta usijitokeze tena Katiba iliyoandikwa mwaka 1992 inaidhinisha muhula wa Rais kutozidi mmoja, Rais Fernando Lugo aliyemtangulia anayetawala sasa aliyeingia madarakani mwaka 2008 na kuhitimisha udikteta wa chama cha Colorado aling’olewa madarakani na Bunge, ambapo mwaka 2012 wabunge wa chama chake cha Liberal na Colorado waliungana kupitisha muswada wa kumng’oa kutokana na mzozo wa wakulima wasiokuwa na ardhi kuondolewa kinguvu kwenye mashamba, ambayo baadaye yalikabidhiwa kwa mwekezaji aliyekuwa swahiba wa dikteta Stroessner aliyewanyang’anya ardhi masikini na kuwapa marafiki zake wakati wa utawala wake.

Migogoro ya ardhi ni donda ndugu nchini humo kwa kuwa asilimia 80 ya ardhi imehodhiwa na mabepari huku wakulima ambao ni wengi hawana ardhi ya kutosha kwa kilimo. Kilichomponza Lugo aliyekuwa Askofu wa Kikatoliki aliyeacha ukasisi na kuingia kwenye siasa akijinadi kuwatetea masikini na kuahidi kuwapa ardhi wakulima, ni kushindwa kutekeleza ahadi alizotoa. 

Nafasi yake ilikaimiwa na Makamu wake Federico Franco hadi mwaka 2013 ulipofanyika uchaguzi uliomweka madarakani Rais Cartes ambaye muhula wake unaisha mwakani, anayetaka kuchezea Katiba ili asalie madarakani kwa kutumia hila na ujanja ikiwamo kujikosha kwa umma kwa hatua yake ya kumshinikiza Waziri wa mambo ya ndani, Tadeo Rojas, kujiuzulu na kumfukuza kazi Kiongozi Mwandamizi wa Polisi Crispulo Sotelo kutokana na mauaji ya mwandamanaji Rodrigo yaliyofanywa na askari polisi Gustavo Florentin.

Hatua alizochukua haziwezi kuwatuliza wananchi wa Paraguay ambao hawataki kurejea upya kwa udikteta kwa njia za kinyemela, bado kuna safari ndefu ya kusaka utangamano kwenye taifa hilo linalotamalakiwa na hamkani inayokosesha shwari kwa vurugu zinazorindima zinazotishia ustawi wake.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles