24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Rais wa Namibia atetea kiti chake

WINDHOEK, NAMIBIA

Tume ya Uchaguzi Namibia (ECN) imemtangaza Rais Hage Geingob wa nchi hiyo kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais kwa kuzoa asilimia 56.3 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi mkuu.

Geingob ambaye alichaguliwa mara ya kwanza kuwa rais wa nchi hiyo mwaka 2014 kwa kupata asilimia 84 ya kura, amepata asilimia 56.3 ya kura na hivyo kuzuia uwezekano wa uchaguzi huo kuingia katika duru ya pili, ambapo angechuana na mwanachama wa chama chake, Panduleni Itula, ambaye amegombea kama mgombea huru.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, Itula amepata asilimia 29.4 ya kura huku kinara wa chama kikuu cha upinzani cha Popular Democratic Movement (PDM), McHenry Venaani akiibuka wa tatu kwa asilimia 5.3.

Baada ya kutangazwa mshindi, rais huyo wa Namibia aliuambia umati wa wafuasi wake katika mji mkuu Windhoek kuwa, “Mimi ni raia wa Namibia mwenye fahari kubwa, kwa namna tunavyofanya chaguzi zetu kwa uhuru na haki, hakuna mapigano, hakuna kushambuliana, kila mtu alikuwa huru kutembea.”

Chama cha SWAPO, ambacho ni chama cha Rais Geingob, kimekuwa madarakani tokea Namibia ipate Uhuru wake kutoka Afrika Kusini mwaka 1990 na bado kinaheshimiwa kutokana na nafasi yake kubwa katika ukombozi wa nchi hiyo.

Hata hivyo, kinara wa chama kikuu cha upinzani, McHenry Venaani aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa, wanatafakari kuhusu kwenda mahakamani kupinga matokeo hayo, akidai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na kasoro nyingi.

Katika uchaguzi wa Bunge, chama tawala kimepata viti 63 kutoka 77 kilivyokuwa navyo, huku chama rasmi cha upinzani cha Popular Democratic Movement (PDM) kikiambulia viti 16.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles