24.8 C
Dar es Salaam
Thursday, September 21, 2023

Contact us: [email protected]

Rais wa Malawi aacha ujumbe wa ushirikiano

 MWANDISHI WETU– DAR ES SALAAM

RAIS wa Malawi, Lazarus Chakwera, ameondoka nchini huku akiacha ujumbe wa ushirikiano, baada ya kumaliza ziara yake ya kiserikali ya siku tatu.

Rais Chakwera aliondoka nchini jana baada ya kufanya mazungumzo na Rais Dk. John Magufuli Ikulu, Dar es Salaam juzi, kisha kuweka jiwe la msingi wa ujenzi wa kituo kipya cha mabasi ya mikoani na nchi jirani, Mbezi Louis jana asubuhi.

Baada ya uzinduzi huo, Rais Chikwera alitembelea ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) katika eneo la Shaurimoyo na Bandari ya Dar es Salaam kujionea maendeleo ya miradi hiyo ambayo inatekelezwa na Serikali.

Ujenzi wa gati la mizigo katika bandari ya Dar es Salaam umekamilika katika eneo lenye uwezo wa kubeba magari 600,000 kwa mwaka.

Akizungumza katika ziara hiyo, Rais Chakwera alisema kuwa Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu kwa maendeleo ya nchi hizo mbili ambapo Watanzania na Wamalawi wanafanya biashara. 

“Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu kwa wananchi wa Malawi kwani inatumika katika maisha yao ya kila siku ya kibiashara kwa kusafirisha mizigo mingi kutoka Tanzania, ikiwemo usafirishaji wa mafuta,” alisema Rais Chakwera.

Alitoa shukrani kwa Tanzania kwani inashirikiana vyema na nchi yake katika masuala ya usafirishaji.

Aliongeza kuwa Tanzania imetoa upendeleo kwa nchi za Kusini mwa Afrika ikiwemo Malawi kwa kutoa eneo la kuhifadhia mizigo kutoka Malawi lililoko Bandari ya Dar es Salaam (Malawi Cargo Centre).

Alieleza kuwa Malawi inaunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania kuimarisha Bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa Bandari ya Mtwara kwani ni muhimu kwa maendeleo ya Malawi hasa kwenye sekta ya usafirishaji. 

“Malawi inaunga mkono juhudi za ujenzi na kuimarisha bandari na huduma za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), hasa kuwepo kwa mchakato wa ufunguzi wa ofisi za TPA mjini Lilongwe, Malawi, hii itawezesha kufanya biashara katika mazingira mazuri baina ya wananchi wa Tanzania na Malawi,” alisema Rais Chakwera.

 Alifurahishwa pia kwa kupata kumbukumbu ya Tanzania kuimarisha mshikamano katika ukombozi wa Afrika hasa nchi za Kusini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles