26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, January 27, 2022

RAIS TREMER ANAPOGEUZIWA KIBAO

MWANAMUZIKI Justin Timberlake alitoa wimbo unaoitwa: ‘What goes around comes around’ (2006), aliouandika akishirikiana na Tim Mosley na Nate ‘Danja’ Hills, lakini yeye si wa kwanza kutoa wimbo wenye maudhui hayo, kwani nyimbo zenye maudhui hayo zinapatikana katika albamu 100 tofauti zikihusisha wanamuziki wengi kwa mashairi yenye matoleo 30,828 duniani kote.

Maudhui hayo ya nyimbo yana umaarufu mkubwa kwa sasa kwenye siasa za Brazil kutokana na mkanganyiko unaofukuta nchini humo, ambapo Rais Michel Tremer aliyechagiza kung’olewa madarakani kwa Rais Dilma Rousseff naye kuwa hatarini kung’olewa na kushadadia ithibati ya mashairi yenye maudhui hayo yanayobainisha kuwa kila kilichojiri hurejea na kujiri upya kwa mara nyingine.

Rais huyo wa Brazil anapinga vikali kuhusika katika kashfa ya kuidhinisha malipo tata kwa Spika wa zamani wa Bunge la awali, Eduardo Cunha, aliyehukumiwa kwa ufisadi.

Ni kioja lakini ndivyo ilivyojiri kwani ilimlazimu Rais Tremer kuhutubia taifa, kupinga taarifa hizo za ufisadi anaotuhumiwa kuufanya zilizochapishwa na gazeti maarufu nchini humo linaloitwa Globo.

Tremer ameruka kimanga kuhusika akibainisha kuwa hatajiuzulu kama waandamanaji wanavyoshinikiza wakichagizwa na wapinzani wake, akipuuzia mbali uwezekano wa kung’olewa madarakani kama alivyochagiza na kumfanyia Rais Rousseff ambaye kilichomng’oa madarakani ni kuchakachua bajeti ya taifa wakati tayari umaarufu wake ukiwa umeporomoka kutokana na matumizi makubwa ya uwekezaji kwenye michuano ya kombe la dunia na mashindano ya Olimpiki pamoja na kashfa sugu ya Petrobras inayohusu visima vya mafuta baharini.

Rais Tremer aliingia madarakani mnamo mwaka mmoja uliopita kwa mujibu wa Katiba ya taifa hilo baada ya kung’olewa Rousseff kwa kuwa alikuwa Makamu wa Rais, lakini inavyoelekea wananchi na wapinzani wake walikuwa wanasubiri fursa ya kumng’oa Rais huyo ambaye anapaswa kutawala kwa miaka miwili na nusu tu kabla ya kufanyika uchaguzi.

Kutokana na hatua zake za kubana matumizi ili kuukarabati uchumi wa taifa hilo zinavyosababisha mbinyo wa ugumu wa maisha kwa wananchi huku nguvu ya uchumi anaotaka kuukarabati ikizidi kudorora kinyume na matarajio yake.

Kwa hiyo kwa sasa Brazil ni kama nchi mbili tofauti kutokana na ongezeko la ukosefu wa ajira kwa watu milioni 13.5 ambao hawapendi hatua zinazochukuliwa na Rais wao.

Lakini upande wa pili masoko ya mitaji na hisa yanafanya vyema zaidi tangu ashike madaraka kwa kufanikisha kudhibiti mfumuko wa bei ingawa kilichopungua gharama hakinunuliki kwani wengi hawana kipato kutokana na kukosa ajira.

Serikali ya Tremer haikosi cha kujitetea kwa kudai kwamba mapato inayokusanya bado hayatoshelezi kiwango cha matumizi makubwa, ikiahidi kukarabati uchumi kwa kuanza na mchakato wa kustaafu kwa wafanyakazi lakini wananchi hawamuelewi, kwani kuna maandamano kadhaa yanayorindima kupinga mkakati huo utakaoongeza umri wa kustaafu ili wafanyakazi wengi wachangie mifuko ya jamii inayotegemewa kwa uwekezaji wa ndani.

Lakini kutabiri mwelekeo wa kukubalika au kutokubalika kwa Rais Tremer ni mtihani mwingine kwani siasa za Brazil wakati mwingine hazitabiriki, licha ya hamkani yote inayomkabili Rais huyo, Serikali yake imefanikiwa kupitisha muswada wa hatua za mabadiliko ya kiuchumi katika Kamati za Bunge la Congress na inatarajiwa muswada huo utapigiwa kura ya kuidhinishwa katika Bunge la awali na kumpa ithibati Rais Tremer, ambaye ndani ya mwaka mmoja wa kuwa madarakani amefanikiwa zaidi kupitisha miswada kulinganisha na mtangulizi wake Rais Rousseff.

Mwenyewe Tremer anajivunia mafanikio yake ya kupenyeza miswada kwa kudai kuwa kutopendwa kwake ndiko kunakompa nguvu zaidi ya kutimiza sera muhimu kwa taifa lake kwamba: “umaarufu utakuja baadaye umuhimu uko kwenye kutimiza mabadiliko ya kuinua uchumi wa nchi, hilo ndilo lengo langu!”.

Ndivyo anavyojinadi Rais Tremer ambaye alichaguliwa kama mgombea mwenza wa Rousseff katika uchaguzi wa mwaka 2014 lakini anashutumiwa kwa kusaliti mapinduzi yaliyomn’goa mtangulizi wake licha ya kuahidi kuachana na siasa ifikapo mwakani.

Mwelekeo wa kudumu au kung’oka kwa Rais Tremer utategemea kama kuna mashiko ya kilichotokea kujiri tena mara nyingine kwani hatua zake zinazomfitinisha na wananchi, zimesababisha Rais wa zamani Luiz Inacio Lula da Silva kujikusanyia umaarufu kwa turufu za uchaguzi mkuu wa mwakani ambao utarudisha uamuzi kwa wananchi tangu kung’olewa kwa Rousseff.

Lula ameshaanza kuchanga karata zake akimshutumu wazi Rais Tremer kwa kupika mapinduzi dhidi ya Roussef ili kutimiza malengo yake binafsi yanayokiuka haki za wafanyakazi, huo ni wimbo mtamu ambao Wabrazil wengi wanapenda kuusikia kwa sasa na kumpa umaarufu Lula ingawa kama ataweza kusimama kugombea Urais kwenye uchaguzi ni suala lingine, kwani anakabiliwa na mashtaka matano tofauti ya ufisadi yanayoweza kumpeleka jela likiwemo sakata la skendo ya Petrobras. Kilichotarajiwa na kinachojiri sasa Brazil vinatofautiana kwani wengi walihisi kuwa kung’olewa kwa Rousseff kungeleta utangamano, lakini taifa hilo linaweza kushuhudia kung’olewa kwa Rais mwingine na kuweka historia ya aliyechagiza kumng’oa mwenzake naye kung’olewa, ikidhihirisha hulka ya muosha huoshwa na kushinikiza maudhui ya wimbo maarufu duniani: ‘What Goes Around Comes Around’.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
176,866FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles