24.4 C
Dar es Salaam
Saturday, September 21, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia Suluhu Hassan awaasa wananchi wa Morogoro kuzalisha mazao kwa wingi

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Morogoro kuzalisha kwa wingi mazao ya chakula na biashara, akibainisha kuwa soko la uhakika lipo. Kauli hiyo aliitoa leo, Agosti 2, 2024, akiwa katika ziara ya siku sita mkoani Morogoro ambapo aliwasisitiza kuongeza uzalishaji wa mazao.

Rais Samia aliwataka wakulima wazalishe zaidi kwa sababu soko lipo. Alisema Tanzania inaweza kujitegemea kwa chakula kwa asilimia 120 kupitia juhudi za wakulima. Kila mkulima anapata chakula cha kutosha kwa mwaka huku asilimia 20 ya mazao ikiwa ni kwa ajili ya kuuza nje ya nchi.

“Tuendelee kuzalisha mazao ya biashara na chakula. Hata mbazi ni zao la biashara. Najua bei ya mbazi katika eneo hili haijawa nzuri, lakini nimemtaka Waziri wa Kilimo kuchukua hatua ili bei ipande kama alivyofanya Kusini mwa Tanzania,” alisema Rais Samia.

Lengo la Ziara

Katika ziara hiyo, Rais Samia aliwashukuru wananchi kwa kuiunga mkono serikali na kudumisha amani na utulivu. “Nimekuja Morogoro kuwaona ndugu zangu tangu nilipokabidhiwa dhamana hii mwaka 2021. Nimekuja kuwasikiliza na kuchukua shida zenu ili tuzifanyie kazi,” alisema.

Pia alisema amekwenda kuona matokeo ya fedha nyingi zinazopelekwa mkoani humo kuondoa changamoto za wananchi na kuzindua, kukagua, na kuweka mawe ya msingi kwa miradi kadhaa inayotekelezwa na serikali, ikiwemo ujenzi wa miundombinu iliyoharibiwa na mvua kubwa za El-nino.

Hospitali ya Wilaya Gairo

Akizindua hospitali ya wilaya ya Gairo, Rais Samia alisema ameridhika na matumizi ya fedha na kazi inayofanywa katika hospitali hiyo. Aliwataka wananchi kuitunza hospitali hiyo ili iendelee kutoa huduma. Pia alimpongeza Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby, kwa kufuatilia maendeleo ya jimbo lake.

Kudhibiti Kukatika kwa Umeme

Rais Samia alisema Gairo walikuwa na changamoto ya kupungua na kukatika kwa umeme, hivyo serikali imejenga ‘Sub-Station’ eneo la Kongwa ili kuwezesha umeme usikatike. “Gridi yetu inayo umeme wa kutosha na njia ya kuleta umeme iko tayari. Tumejenga kituo cha kupooza na kusambaza umeme ili kupunguza kadhia ya kukatika kwa umeme,” alisema.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Rais Samia, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliwataka wananchi kuiunga mkono serikali katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu. Alisisitiza wananchi kupanga safu zitakazokivusha chama katika uchaguzi huo ili CCM iendelee kuwaletea maendeleo.

Daraja la Burega

Akiwa wilayani Kilosa, Rais Samia alizindua daraja la Burega ambalo linaunganisha mkoa wa Tanga na Morogoro. Aliipongeza Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa kuendeleza miundombinu ya barabara kupitia TARURA. Alisema daraja hilo litasaidia kuunganisha wananchi na kurahisisha upatikanaji wa huduma za jamii.

Sekta ya Maji

Rais Samia alikiri kwamba hajafanya vizuri katika sekta ya maji mkoani Morogoro, lakini aliahidi kuwa changamoto hiyo itatatuliwa ndani ya muda mfupi. “Sijafanya vizuri sana kwenye maji Morogoro, lakini miradi inaendelea na ndani ya muda mfupi Morogoro itakuwa na maji safi na salama,” alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa alisema hospitali ya wilaya ya Gairo inatoa huduma zote za upasuaji na majengo yote ya upasuaji yamekamilika. Alisema kazi kubwa ya kizalendo inayofanywa na Rais Samia imegusa maisha ya Watanzania wanyonge.

Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby, aliongeza kuwa serikali ya awamu ya sita imefanya mambo makubwa katika miaka mitatu, ikiwemo ujenzi wa hospitali ya wilaya. Pia alieleza kuwa serikali imetoa zaidi ya bilioni 18 kwa ajili ya miradi ya elimu na afya.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kilosa, Palamagamba Kabudi alisema maendeleo yanayofanywa na Rais Samia hayajawahi kufanyika tangu nchi ipate uhuru. “Rais Samia umewapa matumaini watoto na kuwarejeshea furaha wakinamama wajane,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles