Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa hatua ya kuanza kutekeleza baadhi ya maombi yaliyotolewa na vyama vya wafanyakazi nchini, hususan lile la kuwahamisha watumishi waliokuwa wanalipwa kupitia mapato ya ndani ya halmashauri kwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali (Hazina).
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU), Rashid Mtima, alizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 14, 2024, jijini Dar es Salaam na kufafanua kuwa watumishi 465 ambao ni wanachama wa TALGWU, wameunganishwa kwenye Mfuko wa Hazina.
Mtima alieleza kuwa awali, kulipwa kwa watumishi hao kupitia mapato ya ndani ya halmashauri kulisababisha ucheleweshaji wa mishahara, pamoja na kushindwa kupata huduma za matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutokana na makato kutowasilishwa kwa wakati.
“Hii ni hatua kubwa sana iliyochukuliwa na Serikali ambayo itaondoa kero za muda mrefu, itaongeza ari na morali ya kufanya kazi. Tunashukuru na kuipongeza serikali kwa kuridhia ombi na kilio chetu cha muda mrefu, na kuanza utekelezaji Julai mwaka huu, huku jumla ya wanachama 465 kati ya 648 wameanza kulipwa kupitia Mfuko wa Hazina,” alisema Mtima.
Aidha, Mtima alibainisha kuwa kulikuwa na changamoto za watumishi hao kutokukopesheka katika baadhi ya taasisi za fedha, pamoja na usumbufu walipostaafu kutokana na makato ya michango yao kutowasilishwa kwa wakati kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii.
“Mshahara ndio unaoleta faraja sehemu ya kazi, hivyo tunaishauri serikali iwasimamie wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha mishahara inalipwa kwa wakati kama inavyofanya Hazina,” aliongeza.
Mtima pia alizitaja halmashauri ambazo bado zinalipa mishahara kupitia mapato ya ndani kuwa ni Geita, Ilala, Kinondoni, Mbeya Jiji, Mwanza, Temeke, Dodoma, na Morogoro.
Alisisitiza kuwa endapo halmashauri hizo zitalipa mishahara ya watumishi hao kwa wakati, itaondoa pengo kubwa lililopo katika upatikanaji wa haki na stahiki za wanachama 180 waliosalia, na pia kuondoa matabaka ya kiutumishi mahala pa kazi.
Mtima aliomba serikali kufanya mchakato wa haraka kuhakikisha kuwa wanachama 180 waliosalia katika majiji na manispaa, ambao bado wanalipwa kupitia mapato ya ndani ya halmashauri, nao waanze kulipwa kupitia Hazina ili kuimarisha haki na stahiki zao.