26.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Rais Samia awaonya wakuu wa mikoa kutotumia fedha za anwani za makazi

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema mradi wa mfumo wa anwani za makazi utafanyika kwa utaratibu wa operesheni maalum kama ilivyofanyika katika ujenzi wa madarasa yaliyotokana na fedha za Uviko-19 huku akiwaonya  wakuu wa Mikoa kutotumia fedha za mradi huo kwa ajili ya matumizi ya mengineyo (OC).

Akizungumza leo Januari 8,2022wakati wa kikao kazi na Wakuu wa Mikoa kuhusu mfumo wa anwani za makazi, Rais Samia amesema mradi wa mfumo wa anwani za makazi utafanyika kwa utaratibu wa operesheni maalum kama ilivyofanyika katika ujenzi wa madarasa yaliyotokana na fedha za Uviko-19.

“Fedha tutaleta kwa ukubwa wa mikoa yenu pande zote, fedha hizi sio OC ni ya mradi nyinyi mtaendelea kutumia OC zenu, fedha iende katika miradi,”amesema Rais Samia.

Aidha, ametoa wito kwa Tamisemi  kuendelea kuwashirikisha wananchi na kuhakikisha mradi huo unawekwa na kuwahudumia wananchi kwa urahisi ambapo amedai ushirikishwaji utawafanya wawe walinzi wa miundombinu.

Rais Samia pia awaagiza viongozi kuwashirikisha watanzania kwa kuwafundisha kuhusu umuhimu wa mradi huo wa anwani za posta na makazi ili waweze kuwa na uelewa na kushiriki ipasavyo ambapo amedai  mradi huo unatakiwa kukamilika itakapofika Mei mwaka huu.

“Kama hamkumaliza zoezi au halikwenda vizuri tutakaa ana kwa ana, ukiwa na changamoto zake tuzungumze ukikaa nazo hadi muda ukamalizika itabidi tukae ana kwa ana tuelezane,”amesema Rais Samia na kuongeza:

“Maeneno mengine kimebandikwa kibati mtu anajua namba yangu ni hii sasa kwa kuanzia sasa hivi tusijiingize gharama za vibati mwenye nyumba anapara vizuri anapaka chokaa unaandika kama chokaa nyeupe unaandika kwa rangi nyeusi 115 si itakuwa imeishakaa?

“Sasa zile gharama za vibati zinaondoka twendeni kienyeji kwa kupunguza gharama lakini gharama zinapungua, Mawaziri mnaohusika mlisimamie hilo,”amesema.

Kwa upande wa Serikali kuu, Rais Samia amesema watahakikisha wanatekeleza maelekezo kama yalivyo kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM pamoja na kuunganisha miundombinu migumu na laini hasa kwenye mifumo ya mitandao.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango amesema mfumo wa makazi ni nyenzo muhimu hivyo amewaomba viongozi kuwaelekeza wananchi jinsi ya kutumia mfumo huo kwa lengo la kuhakikisha mradi unafanikiwa.

Naye, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemhakikishia Rais Samia kwa kudai wanaenda vyema katika zoezi la sensa ya watu na makazi ambapo amedai ndio maana zoezi hilo walilipeleka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) lengo likiwa ni kuanzia ngazi ya chini.

Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah amesema SMZ na SMT wapo tayari kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa kiwango kikubwa huku akiwataka watendaji kulisimamia jambo hilo.

Awali, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnaye amesema wapo tayari kupokea maelekezo ya rais juu namna gani ya kufanya ili mradi huo uzidi kuleta tija kwa Watanzania.

Amesema awali walipanga mradi huo utumie zaidi ya Sh bilioni 700 lakini kwa sasa utatumia Sh bilioni 28, hivyo kuokoa zaidi ya Sh bilioni 660.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles