Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan leo Oktoba 10, 2023 ametunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima (Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Jawarhalal Nehru, Delhi India.
Rais Samia ametunukiwa PhD hiyo kwa mchango wake kwenye diplomasia ya uchumi; kwa kuwa chachu ya maendeleo yanayogusa wananchi moja kwa moja; na kwa kuimarisha uhusiano wa kimataifa.
Mara baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Rais Samia ameitunuku kwa mabinti wa Tanzania wanaoishi katika mazingira magumu, akiwasihi kutokata tamaa kutokana na mazingira waliyopo na kuitaka jamii kushirikiana kuwawezesha watoto hao kufikia ndoto zao.
Tangu kuingia madarakani Rais Samia ameweka jitihada kusaidia watoto wakike ikiwa ni pamoja na kuruhusu wanafunzi waliojifungua kuruhusiwa kuendelea na masomo.
Rais Samia anakuwa mwanamke wa kwanza kutunukiwa shahada hiyo ya heshima na chuo hicho maarufu duniani.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1969, ni viongozi wawili tu ambao wamewahi kutunukiwa shahada hiyo: Rais wa Urusi, Vladmir Putin pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan Hayati Shinzo Abe.