Na Brighiter Masaki, Mtanzania Digital
Rais Samia Suluhu Hassani amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuanza kuwapanga upya wafanyabishara wadogo maarufu machinga kutokana na kuzuia maduka ya watu na kuifanya Serikali kupoteza kodi.
Ametoa agizo hilo leo Septemba 13, wakati akiwaapisha mawaziri wapya walioteuliwa jana ambao ni January Makamba (Waziri wa Nishati), Dk. Asha Kijatu (Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari), Prof. Makame Mbarawa (Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi) na Dk. Stergomena Tax (Waziri wa Ulinzi).
Rais Samia amewataka wakuu wa mikoa hao kuwapanga wamachinga katika maeneo yatakayoondoa kero kwa watumiaji wa njia pamoja na wamiliki wa maduka ambao hivi karibuni wametoa malalamiko kuwa wanakosa mapato kwa sababu biashara wanazofanya zinafanana na za machinga ambao hawalipi kodi.
“Najua kwamba Serikali tumetoa fursa kubwa kwa machinga kufanya biashara zao ili kujiingizia vipato vyao. Wakuu wa mikoa na wilaya wanawapanga lakini imefika wakati wameenea kila mahali, mpaka kwenye maduka wao wanaziba na wenye maduka hawauzi.
“Wenye maduka nao wanaamua kutoa bidhaa kwenye maduka yao na kuwapa machinga, hili linaikosesha Serikali mapato kwa sababu machinga halipi kodi lakini mwenye duka anatakiwa kulipa kodi.
“Naomba wakuu wa mikoa mchukue hatua mapema za kuwapanga machinga, sitaki kuona ninayoyaona kwenye TV, ngumi, kupigana, kuchafuliana, vyakula kumwagwa hii hapana, naomba mchukue hatua vizuri za kuwapanga bila kuudhi wenye maduka wala machinga.
“Nitoe wito kwa machinga na wajitahidi kufuatia sheria zilizowekwa na kufuata yale wanayoelekezwa na wakuu wao wa mikoa. Niwatakie kazi njema mlioapa leo na wale mlioko kazini mkaendeleze kazi, nami nakwenda kendelea na kazi ya marekebisho,” amesema Rais Samia.