Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
RAIS Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki ina uwezo wa kuzalisha chakula kingi mara mbili ya kinachozaliwa sasa, iwapo kutakuwa na mikakati madhubuti.
Akizungumza katika mkutano wa 22 wa wakuu wa nchi saba za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ulioanza leo Julai 21, 2022 jijini Arusha, Rais Samia amesema EAC ina ardhi kubwa na ina uwezo wa kuzalisha chakula zaidi kuliko kinachozalishwa sasa.
Nafikiri tuangalie namna tunavyoitumia hiyo ardhi katika kuzalisha. Ardhi pekee haiwezi kufanikisha hilo, lazima tuangalie maji kupitia kilimo cha umwagiliaji je tutavunaje maji ya mvua. Hatuvuni maji ya mvua,” amesema Rais Samia.
Amesema ni lazima kuwe na skimu za umwagiliaji zitakazowezesha kilimo badala ya kutegemea mvua na kwamba, ili kuzalisha zaidi ni lazima jumuiya hiyo iangalie uwekezaji katika kilimo na kuwawezesha wakulima kuzalisha zaidi kupitia kilimo cha kisasa.