Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
*Aahidi Milioni 20 kwa goli la ushindi
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ameibeba tena klabu ya Yanga, akisema kuwa katika mechi za fainali ya Kombe la Shirikisho itakayopigwa Mei 28 na marudiano ni Juni 3, kila bao la ushindi atalipa Sh milioni 20, sambamba na kutoa ndege ya Serikali kuipeleka timu hiyo nchini Algeria kwa ajili ya kumenyana na wapinzani wao USM Alger.
Timu mbili hizo zinatarajiwa kukwaana katika mechi mbili za fainali ya Kombe la Shirikisho, mechi inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Yanga na Watanzania kwa ujumla kuishuhudia ikiweka historia ya kutwaa taji hilo linaloratibiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Akizungumza katika tukio la uzinduzi wa Mradi wa Minara ya kurusha matangazo ya Televisheni ardhini (DTT) ya Kampuni ya Azam, Rais Samia alisema uamuzi huo unatokana na matamanio yake ya kuona timu ya Tanzania inafanya vizuri katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
“Nilianza kwa kutoa Sh milioni 5 kila goli kwa timu ya Simba na Yanga kwenye michuano hii, lakini pia nikatoa Sh milioni 10 kila goli moja ambapo bahati mbaya Simba wao wameishia njiani na kuwaacha wenzao Yanga.
Uamuzi wa Rais Samia kutoa mamilioni kwa timu za Simba na Yanga umechangia kwa kiasi kikubwa kuzipaisha timu hizo sambamba na kutangaza soka la Tanzania, ambapo Yanga kwa mara ya kwanza ikifanikiwa kufuzu hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho.