24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia aagiza halmashauri kuwatengea machinga maeneo rafiki

Clara Matimo na Sheila Katikula, Mwanza

Rais Samia Suluhu Hassan, ameziagiza halmashauri zote nchini kuwatengea wafanyabiashara wadogo (machinga),  maeneo yanayofikiwa na watu   ili waweze kunufaika na biashara zao, badala ya kuwapeleka katika maeneo ya mapori.

Pia amewata machinga kutotumika kwa wafanyabiashara wa kati maana baadhi yao wamekuwa wakichukua bidhaa za kundi hilo na kuwauzia kwenye maeneo yao hali inayosababisha kuikosesha Serikali mapato.

Akizungumza na Vijana katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza Juni 15 mwaka huu katika mkutano uliolenga kujadili fursa mbalimbali za kumkomboa kijana,  Rais Samia amesema Serikali inajenga masoko na standi katika kila mkoa ili kutenga maeneo kwa ajili ya machinga waweze kufanya biashara bila kubugudhiwa lakini baadhi ya watendaji wamekuwa wakiwapeleka katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi.

 “Lakini pia tumehimiza halmashauri kutenga maeneo maalum ambayo yanafikiwa na watu  ili vijana hao machinga wakakae na wafanye biashara zao, pamoja na maelekezo hayo,  juzi niliona  pale Morogoro machinga wametengewa maeneo ya nje ya mji ambako watu hawafiki na kwa sababu hawauzi wamerudi maeneo waliyoondoshwa.

“Niliona mgambo wakiwavamia wakawapiga na kuharibu vitu vyao, nimesikitishwa sana na tukio hilo, na niseme hapa mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa eneo lile hawana kazi,”alisema Rais Samia ambaye alishangiliwa na umati wa vijana waliofulika uwanjani hapo kumsikiliza.

Rais Samia aliongeza”Kwa sababu kuna njia nzuri zaidi ambayo wangeitumia kusema nao na wakawaondowa kwa usalama lakini si picha ile nilioiona kwenye TV, kwa hiyo nakuagiza Waziri wa Tamisemi ulishughulikie suala hilo,”aliagiza.

“Nanyi watoto wangu machinga nawasihi sana msitumiwe na wafanyabiashara wenye maduka, mnapochukua bidhaa zao na kuwauzia kumbukeni hamtoi risiti hivyo mnaikosesha Serikali mapato maana fedha tunazopata kutoka kwa wafanyabiasharawanazolipa ushuru ndizo tunazozitumia kuwaboreshea maeneo ya kufanyia biashara pamoja na kutatua changamoto mbalimbali hivyo nawaomba msitumike kabisa,”alisema.

Awali akifungua mkutano huo wa kujadili fursa kwa vijana,  Rais Samia alisema Serikali imejikita kuboresha elimu na ujuzi, ili kuwawezesha vijana kujiajiri wanapohitimu katika ngazi mbalimbali za elimu, badala ya kutegemea kuajiriwa.

Aidha aliwataka vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kujiingizia kipato badala ya kuilaumu na kuishutumu Serikali, “Kama unalaumu laumu na utoe mapendekezo nini kifanyike  ili kutatua changamoto ya lawama unazotoa na kama ukishutumu toa ushahidi ili tuchukue hatua,”alisisitiza Rais Samia.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Ajira, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema vijana 64,000 watanufaika kwa kupata elimu bure ya ufundi kutoka vyuo vya ufundi hadi sasa waliokwishapata elImu hiyo ni 14,000 lengo la Serikali ni kuwawezesha ili wajiajiri.

Nao baadhi ya vijana waliohudhuria mkutano huo akiwemo Goodluck Lingo, Kazilahabi Kalenga na Meshack Mpalanga walisema changamoto zinazowakabili ni pamoja na ukosefu wa mitaji moja ya sababu ikiwa ni viwango vikubwa vya riba kutoka taasisi za fedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles