waandishi wetu –Dar/Dodoma
RAIS Dk. John Magufuli amesema pamoja na jitihada zinazofanywa na mabeberu na vibaraka kumkwamisha katika utendaji wake wa kazi, kamwe hatakata tamaa.
Alitoa kauli hiyo jana jijini Dodoma katika mahafali ya 10 ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), yaliyohudhuriwa na watu wa kada mbalimbali.
Katika mahafali hayo, wahitimu 6,488 walipatiwa vyeti mbalimbali akiwemo Rais Magufuli ambaye alitunukiwa shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa.
“Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, changamoto hazikosekani na changamoto hizo na vikwazo ni pamoja na jitihada zinazofanywa na mabeberu na vibaraka wao kwa kuwatumia wa ndani kujaribu kuweka vikwazo ili malengo yetu yasitimie.
“Ninyi ni mashahidi, ndiyo maana mmekuwa mkisikia hiki na kile, mara kuna ugonjwa huu mara kuna nini, yote hayo ni kujaribu kutukwamisha, mimi sitakata tamaa na leo (jana) mmenipa hii heshima, sitakata tamaa kabisa,” alisema Rais Magufuli.
Alisema katika kipindi cha miaka minne aliyokuwa madarakani, amejifunza namna ya kuvishinda vikwazo hivyo.
“Kwa miaka minne niliyokuwa madarakani nimejifunza namna ya kuvishinda vikwazo hivyo na uwezekano upo mkubwa sana ikiwa tu sisi Watanzania tutakuwa wamoja na kutanguliza uzalendo mbele na kushikamana,” alisema Rais Magufuli.
Pamoja na hilo, Rais Magufuli alisema siku alipopokea barua ya kutunukiwa shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa kutoka kwa mkuu wa chuo hicho, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, alipata shida kwa sababu hajazoea vya bure.
“Napenda nikiri kwamba siku nilipopata barua kutoka kwa makamu wa chuo mzee Mkapa, kuwa chuo kimenipa shahada ya heshima ya falsafa, nikajiuliza maswali mengi sana na sikupata majibu haraka, swali la kwanza lilikuwa kwanini mimi, kwanini sasa kwa sababu mimi nimekuwepo siku zote, kwanini nipate shahada ya bure ya bila kusota.
“Sasa baada ya kupewa barua hii nilikaa mwezi mzima bila kujibu, baadaye wasaidizi wangu walinifuata wakanikumbusha kuwa bado sijajibu barua ya mzee Mkapa, nikawaambia nitajibu, bado nikachelewa, hii ni kwa sababu dhamira yangu ilikuwa inanisuta kwamba kwanini nipewe cha bure.
“Shahada hii ya heshima unaheshimiwa tu halafu unapewa na wewe unajishangilia, sasa mimi nilijiuliza maswali hayo kutokana na maisha niliyolelewa na mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, sikuzoea kupewa vitu vya bure au vya dezo kwa kiswahili cha mjini.
“Nakumbuka zamani wakati nikiwa mwanafunzi hata nikienda kwa baba yangu kuomba hela ya kalamu, alikuwa hanipi kirahisirahisi, alikuwa akinipa kwanza shughuli za kufanya au kuchunga ng’ombe au kwenda kuuza maziwa au kazi yoyote ambayo atajua umesota kidogo, hata akikupa hela ya kalamu anajua kuwa umesotea.
“Baba yangu hakupenda vya bure, hivyo ndivyo nilivyolelewa ingawa nikiri wakati ule sikumwelewa, nilimwona baba yangu ni mkoloni sana, lakini nilipokua na leo nimekuwa Rais ndiyo nimeelewa kwamba hapa duniani hakuna vya bure na mtu akikupa cha bure lazima ujiangalie vizuri.
“Maana hivi vya bure ni vya kuviogopa kabisa, mtu akikupa cha bure lazima ujiulize mara mbilimbili kwanini anakupa, mwingine anaweza kujifanya anakupa cha bure kumbe kuna kitu anakitaka kutoka kwako.
“Vya bure vinatesa, vya bure sio vizuri, tena inawezekana mzee Bure alishakufa zamani, unaweza kujiuliza mtu kama mimi nisiyependa vya bure ila umeandikiwa barua na Rais Mkapa aliyewahi kuniteua kuwa waziri, nilikaa mwezi mzima sijajibu ile barua ya kutaka nitunukiwe shahada.
“Lakini kumbe shahada hii imetolewa kutambua mafanikio yaliyopatikana katika Serikali ya awamu ya tano na mafanikio haya hayakupatikana kwa juhudi zangu mwenyewe bali kwa ushirikiano wa Watanzania,” alisema Rais Magufuli.
TAFITI ZA KUPUNGUZA UTEGEMEZI
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alivitaka vyuo vikuu nchini kufanya tafiti mbalimbali kulingana na mahitaji na vipaumbele vya nchi na kupunguza kutegemea misaada ya nje kwenye tafiti hizo kwa kuwa wanaotoa misaada ndio wanaowapa ajenda za utafiti.
“Ili kukuza uwezo wa kujitegemea katika gharama za utafiti, anzisheni na imarisheni mifuko yenu ya fedha za utafiti, tafuteni njia mbalimbali za kuimarisha mifuko hiyo, ikiwemo kutumia taaluma zenu mlizonazo.
“Serikali kwa upande wake itaendelea kusaidia kwa kuongeza mchango wake katika mfuko wa utafiti wa kitaifa nchini, kwa kushirikiana na jitihada za vyuo vikuu katika kuimarisha uwezo wetu wa ndani wa kugharamia tafiti zetu zinazobeba ajenda zetu wenyewe.
“Tafiti na matokeo ya tafiti hizo zitakuwa na maana tu ikiwa zitasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wetu, angalieni namna tafiti zenu zinavyoweza kukabiliana na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa dira ya maendeleo ya taifa.
“Pia bainisheni matatizo na tafuteni majibu kwa yanayowakabili wazalishaji mbalimbali kama vile wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji madini na wenye viwanda,” alisema Rais Magufuli.
Vilevile alisema ni lazima vyuo vyote nchini viwe chimbuko la maarifa mapya na chachu ya maendeleo.
Alisema haitasaidia endapo matokeo ya tafiti, maarifa, ujuzi na mbinu zinazozalishwa vyuoni havitatumiwa na Watanzania na kwamba Serikali ya awamu ya tano imejitahidi kutumia wataalamu wa ndani katika kutafuta majibu ya mambo mbalimbali.
WATANZANIA HAWAPASWI KULALAMIKA
Aidha Rais Magufuli alisema Tanzania ni tajiri na Watanzania hawapaswi kulalamika bali wanatakiwa kuulinda kwa nguvu zote utajiri ambao upo.
“Nchi yetu ni tajiri na hatutakiwi kulalamika, haya yote tukiyafanya kwa pamoja yatatupa fursa kubwa kwa mchi yetu kujikomboa kiuchumi.
“Lakini kama mjuavyo fursa zitokanazo na utajiri huu wa rasilimali hizi ni muhimu wakati wote ziwe chini ya udhibiti wa kwetu wenyewe ili ziweze kutunufaisha, ndiyo maana mwaka juzi tulifanya marekebisho ya sheria zetu na tumeanza kupata mafanikio makubwa,” alisema Rais Magufuli.
Alisema tangu kupitishwa kwa sheria za madini, makusanyo yameongezeka kutoka Sh bilioni 191 mwaka 2016-17 na kufikia Sh bilioni 335 kwa mwaka wa fedha uliopita, na kwa mwaka huu wanatarajia kukusanya Sh bilioni 445.
UDOM WAOMBA BILIONI 730/-
Naye makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Faustine Bee alimwomba Rais Magufuli Sh bilioni 735 kwa ujenzi wa ndaki mbili na ukarabati wa ukumbi wa Chimwaga.
Profesa Bee alisema ujenzi wa ndaki hizo unahitaji Sh bilioni 731 na kwamba kukamilika kwake kutafanikisha lengo la kudahili wanafunzi 40,000 kwa mwaka.
Alisema tathimini iliyofanywa na Wakala wa Majengo nchini (TBA) kuhusu ukarabati wa ukumbi wa Chimwaga kuwa wa kisasa, imeonyesha zinahitajika Sh bilioni 14.
Aidha Profesa Bee alisema kwa mara ya kwanza wahitimu wa shahada ya udaktari walipata vyeti vyao jana na wahitimu wengine watapatiwa Jumatatu baada ya kukamilisha taratibu zinazotakiwa.
“Vyeti hivi vimeongezewa alama za siri ili kutoghushiwa. Katika mwaka wa masomo 2019/20 tumedahili wanafunzi 9,674 kati ya 15,000 waliopanga kudahiliwa sawa na asilimia 64.5.
“Na kuanzia Januari mwakani utaratibu wa chuo kuwapangishia nyumba za kuishi watumishi wake utakoma na badala yake kitawapatia fedha wanaostahili,” alisema Profesa Bee.
SABABU ZA KUMPA SHAHADA JPM
Kuhusu shahada aliyotunukiwa Rais Magufuli, Profesa Bee imetolewa kutokana na uongozi wake uliotukuka hususan katika ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuwekeza katika elimu, miundombinu, mawasiliano, nishati, utalii na kuimarisha utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa.
“Shahada kama hii pia imewahi kutolewa kwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete mwaka 2010 na waziri mkuu wa zamani, marehemu Rashid Kawawa naye amewahi kupewa shahada ya namna hii,” alisema Profesa Bee.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Gaudensia Kabaka, alisema mabadiliko ya muundo yameokoa Sh milioni 432 za uendeshaji kwa mwaka.
Alisema katika mabadiliko hayo wamepunguza idara kutoka 62 hadi 30 na wajumbe wa vyombo vya uamuzi kutoka 1,365 hadi 743.
Kabaka ambaye alipata kuwa Waziri wa Kazi na Ajira katika Serikali ya awamu ya nne, aliwataka wahitimu 6,488 kushinda vishawishi vinavyoweza kuwa kikwazo kwao.
Habari hii imeandaliwa na ELIZABETH HOMBO (Dar) NA RAMADHANI HASSAN (Dodoma)