ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli amesema wakati akiwa Naibu Waziri wa Ujenzi katika Serikali ya awamu ya tatu, alinyweshwa sumu kutokana na utendaji wake wa kazi.
Alitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Rais mstaafu Benjamin Mkapa kilichoelezea maisha yake.
“Tulipofanya kazi vizuri kwenye kujenga barabara, mzee Mkapa alifurahi sana, akatamka kwamba mimi ni askari wake wa mwavuli namba moja, ameligusia hili kwenye ukurasa wa 107 wa kitabu chake.
“Licha ya nia yake njema, iliniletea shida mimi binafsi na sitasahau hili maishani mwangu, mawaziri tena wa ngazi za juu wakaanza kunichukia.
“Baada ya chuki zilizosababishwa na mzee Mkapa kunisifia, nilipewa sumu Dodoma almanusura nifariki dunia, lakini nikanusurika.
“Nikamweleza mzee Mkapa dhamira yangu ya kutaka kujiuzulu, aliniangalia kwa jicho la baba na mwana na kunihurumia sana, hili halijawahi kusemwa popote, nimeona niseme leo kwa kuwa ni siku ya mzee Mkapa.
“Baadaye nilipokuja kumwambia mzee Mkapa kuwa nataka kujiuzulu baada ya kupewa sumu, akaniambia ‘John kafanye kazi, kamtangulize Mungu’,” alisema Rais Magufuli.
Aliendelea kusimulia kuwa baada ya hapo, akapewa ulinzi na akaendelea kuchapa kazi.
“Katika tukio hili nilimuona mzee Mkapa kuwa ni mtu anakupa matumaini hata kama umekata tamaa,” alisema.
Mbali na hilo, Rais Magufuli alikiri kuwa Mkapa ni mfano wake wa kuigwa huku akimshukuru kwa mchango wake katika safari yake ya siasa na uongozi kuanzia mwaka 1995 alipomnadi katika kampeni za Uchaguzi Mkuu akigombea ubunge.
“Nakumbuka siku ya kwanza nagombea ubunge mwaka 1995, mzee Mkapa alininyanyua mkono akawaambia wananchi kuwa ‘nileteeni kijana huyu’ na kweli nikashinda ubunge.
“Baadaye akaniteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na baadaye Waziri wa Ujenzi, pia alikuwa akikubali ushauri wangu, nikiwa katika nyadhifa hizo na alinitia moyo katika uamuzi wangu wa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015,” alisema.
Katika hotuba yake, Rais Magufuli alimpongeza Rais mstaafu Mkapa kwa kuandika kitabu hicho kuhusu maisha yake kuanzia alipozaliwa mwaka 1938 katika Kijiji cha Lupaso, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, safari yake ya masomo, siasa na urais.
Alisema kitabu hicho kitawasadia Watanzania na watu wengine duniani kujifunza na kufahamu mchango alioutoa kwa taifa na katika jumuiya ya kimataifa katika masuala ya maendeleo na uongozi.
Rais Magufuli alisema miongoni mwa ushauri ulioungwa mkono na Rais mstaafu Mkapa ni Serikali kuanza kujenga barabara za lami kwa fedha za ndani kwa kutenga Sh bilioni 1.85 kila mwezi na kusimamia kwa karibu utendaji wa wizara hali iliyosababisha aitwe jina la utani la askari wa mwamvuli.
Pia alimpongea Mkapa kwa mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania na kupiga vita umasikini kwa kuanzisha mikakati mbalimbali ikiwemo Mkakati wa Kukuza na Kuondoa Umasikini Tanzania (Mkukuta), Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM).
Vilevile alieleza furaha yake na juhudi zilizofanywa na Mkapa katika kukuza uchumi, kuondokana na utegemezi na kudumisha amani na kwamba ni kutokana na hilo hata Serikali ya awamu ya tano anayoiongoza inasimamia mwelekeo huo.
Pamoja na kuipongeza Taasisi ya Uongozi kwa kuandika kumbukumbu za viongozi, ameitaka kuchapisha kitabu cha maisha binafsi ya Rais mstaafu Mkapa kwa lugha ya Kiswahili ili Watanzania wengi waweze kusoma.
Aidha aliwataka viongozi wengine wakiwemo wa ngazi za chini kuandika vitabu kuhusu maisha yao.
Rais Magufuli pia alisema akiwa naibu waziri wakati huo wa uongozi wa Mkapa, makatibu wakuu walikuwa hawamheshimu, lakini alikuwa bega kwa bega na yeye.
“Makatibu wakuu huwa hawaheshimu manaibu mawaziri, lakini wakati ule nikiwa naibu waziri nikiona katibu mkuu hanisikilizi, Mkapa alikuwa bega kwa bega na lengo lake ilikuwa ni hakuna kiongozi aliye juu ya mwingine,” alisema Rais Magufuli.