32.2 C
Dar es Salaam
Thursday, February 2, 2023

Contact us: [email protected]

Rais Magufuli nenda kawatembelee Kagera

Rais John Magufuli
Rais John Magufuli

NA PETER MITOLE,

KUNA uwezekano kuwa wito ninaoutoa kupitia safu hii leo ukawa unausoma ukiwa umepitwa na wakati. Hii ni kwa sababu wakati naandika haya kile ninachokisema humu kilikuwa hakijatokea.

Nacho ni kumshauri Rais John Magufuli kufanya hima kuwatembelea watu wa Mkoa wa Kagera na jirani zao ambao takribani wiki mbili zilizopita walipatwa na janga kubwa la tetemeko la ardhi. Ni tetemeko kubwa ambalo halijawahi kutokea nchini.

Ukubwa wake unathibitishwa si tu na vipimo vya kisayansi, bali pia na kwa uharibifu ambao tetemeko hilo lilisababisha ikiwamo vifo vya watu 19 na kujeruhi mamia wengine.

Uharibifu wa mali na miundombinu ni mkubwa kiasi kuwa hadi hivi sasa imekuwa vigumu, hata kwa kukadiria tu, kufahamu thamani yake halisi.

Ni ukubwa wa janga hilo ndio ulimfanya Rais Magufuli kuahirisha safari yake nchini Zambia hivi karibuni. Aliamua kubaki nchini ili kulishughulikia tatizo hilo kwa ukaribu zaidi.

Hilo ni jambo la kupongezwa sana kwa sababu ni uamuzi wa busara unaotoka kwa kiongozi unaoonyesha kuwa kweli anawajali watu wake.

Ninaamini kuwa katika kipindi cha takribani wiki mbili zilizopita, Rais Magufuli amefanya mambo mengi makubwa katika kushughulikia madhara ya tetemeko hilo.

Ninaamini kuwa chini ya uongozi wake, misaada mingi inayohitajika kuwasaidia waathirika wa tetemeko hilo imepatikana na itaendelea kupatikana. Lakini pamoja na mambo hayo makubwa aliyoyafanya, bado Rais Magufuli amebakiza jambo moja, nalo ni kuwatembelea na kuwafariji wananchi wake mkoani Kagera.

Kuna watu ambao wanaweza kuona kuwa anachokifanya Rais Magufuli ni kikubwa kuliko kuwatembelea watu wa Kagera. Inaweza kuwa hivyo, lakini kuwatembelea waathirika hao na kuwafariji ni jambo kubwa sawasawa au pengine kuzidi yale ambayo anayafanya kukabiliana na tukio hilo.

Ni kuonyesha ubinadamu kwa kiwango cha juu kabisa.

Ni kweli kuwa Rais amepokea taarifa za kina kuhusiana na tetemeko hilo na hatua ambazo zimechukuliwa hadi sasa kukabiliana na madhara yake, lakini ninaamini kuwa atapata muono wa ziada iwapo yeye mwenye atajionea kwa macho yake kile kilichoukumba Mkoa wa Kagera na majirani zao. Kuona ni kuamini na hapo ndipo unapokuja umuhimu wa Rais Magufuli kutembelea Kagera.

Lakini, katika mila na utamaduni wetu, ni jambo zuri sana kuhani msiba. Na kila inapowezekana, kuwatembelea wafiwa kwa lengo la kuwapa pole ni jambo linalopendekezwa. Kagera imepatwa na msiba mkubwa na hivyo ni busara kwa kiongozi wao kuwatembelea ili kuwapa pole.

Hata kama Rais Magufuli anaielewa fika hali ya Kagera kutokana na taarifa alizozipokea hadi hivi sasa, naamini wananchi wa Kagera watafarijika sana pale watakapomwona kiongozi wao mkuu, akiwapa mkono wa pole wafiwa moja kwa moja.

Lakini pia umuhimu wa Rais Magufuli kutembelea Kagera ili kuonyesha msisitizo wa yale aliyoyasema kuhusiana na hatua ambazo zinachukuliwa kukabiliana na matokeo ya tetemeko hilo.

Rais ameomba misaada zaidi kwa waathirika lakini pia Rais ameonya watu wenye lengo la kuitumia misaada hiyo kujinufaisha binafsi.

Maonyo na maombi yake yatakuwa na uzito sana pale atakapoyatoa akiwa amezungukwa na familia zilizopoteza wapendwa wao kwenye tukio hili kubwa. Maombi na maonyo haya ya rais yatakuwa na uzito mkubwa sana iwapo atayatoa akiwa amezungukwa na vifusi vya nyumba zilizobomolewa na tetemeko hilo.

Ndio maana namwomba kwa unyenyekevu rais wangu afanye hima, afunge safari kuwatembelea wananchi wa Mkoa wa Kagera na majirani zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles