28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

RAIS MAGUFULI, MUSEVENI WAFUNGUA FURSA

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA


MAZUNGUMZO kati ya Rais Dk. John Magufuli na Rais Yoweri Museveni wa Uganda yamefungua ukurasa mwingine wa ushirikiano katika sekta zaidi ya tano kwa nchi hizo.

Hayo yalibainika juzi mjini hapa, kwenye mkutano wa kwanza wa ushirikiano kati ya wataalamu kutoka nchi hizo mbili.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi, alisema nchi hizo zinatarajia kuanza ushirikiano katika maeneo muhimu.

Aliyataja maeneo hayo yatakayojadiliwa na wataalamu kisha kusaini makubaliano ya ushirikiano kuwa ni pamoja na sekta ya biashara, kilimo na mifugo, usafiri wa anga, majini na reli.

“Mkutano umekaa muda mrefu bila kufanyika, lakini kutokana na maelekezo ya wakuu, tumelazimika kufanya mkutano haraka ili kufikia uamuzi wa masuala mbalimbali.

“Tumeingia makubaliano haya na Uganda mwaka 2017 na tangu wakati huo, hatujakutana na leo tunakutana hapa tukiwa tumeweka mkazo mkubwa katika kufikia makubaliano.

“Majadiliano hayo yameshirikisha washiriki 40 wa hapa nchini na wengine 26 kutoka Uganda wanaotoka katika sekta mbalimbali,” alisema Mwinyi.

Katika maelezo yake, Mwinyi alilitolea mfano eneo la utangazaji ambapo alisema wataalamu kutoka idhaa za utangazaji za Tanzania na Uganda wanatarajia kujadiliana kwa kina juu ya eneo hilo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Wizara ya Nje nchini Uganda, Patrick Mugoya, aliwashukuru wakuu wa nchi hizo mbili, akisema uamuzi huo utarejesha ushirikiano wa kindugu baina ya nchi hizo.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Rais Museveni alifanya mazungumzo na Rais Dk. Magufuli na kukubaliana kuanzisha ushirikiano katika sekta mbalimbali.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles