23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

RAIS MAGUFULI MPENDE ADUI YAKO 

RAIS John MagufuliRAIS John Magufuli ameyashutumu magazeti mawili, akiyaambia kuwa siku zake za kuendelea kufanya kazi zinahesabika. Ametoa kauli hiyo kwa maelezo kuwa magazeti hayo yamejikita katika kuandika habari za uchochezi.

Kwa bahati mbaya, Rais Magufuli hakuyataja magazeti hayo wala habari za uchochezi zilizokuwa zikiandikwa na magazeti  hayo. Hivyo, inakuwa vigumu sana kufahamu kwa uhakika aina ya uchochezi ambao magazeti hayo yameufanya kiasi cha kumchukiza Mkuu wa Nchi.

Hata hivyo, naamini kuwa hatua ambazo Rais Magufuli ameahidi kuzichukua dhidi ya magazeti hayo ni kali mno na hazistahili. Hatua hizo hazistahili kwa sababu naamini kuwa hazitasaidia katika jitihada za Rais Magufuli kuibadilisha Tanzania.

Ni kweli kuwa magazeti yanayofanya uchochezi ni hatari sana kwa mustakabali wa nchi, lakini hiyo haiondoi umuhimu wa vyombo vya habari katika nchi yoyote ile wala si tiketi ya kuanza kuvishughulikia vyombo vya habari.

Sote tunafahamu jinsi ambavyo vyombo vya habari vilivyosababisha madhara makubwa katika nchi kadhaa, lakini kuvichukia vyombo hivyo ni sawa na kujichukia mwenyewe kwa sababu bado umuhimu wa vyombo vya habari katika kufanikisha maendeleo ni mkubwa.

Pamoja na hayo, ninaamini katika umuhimu wa mtu kupatana na mgomvi wako bila kusababisha msuguano baina yenu. Hilo ni muhimu sana katika mazingira ambayo pande hizo mbili zinategemeana kama vile ilivyo kwa Serikali ya Rais Magufuli na vyombo vya habari.

Ninaamini kuwa vyombo vya habari ni moja ya nyenzo ambazo Rais Magufuli na Serikali yake wanavitegemea ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu na mipango ambayo imepangwa kwa ajili ya kuleta maendeleo nchini. Ninaamini pia Serikali ni muhimu sana katika ustawi wa vyombo vya habari.

Hivyo, kwa namna hii ya utegemezi ambayo kila upande unao kwa mwenzake, ni vema pande hizo kila mara zikatafuta namna bora ya kufanya kazi pamoja. Hilo litawezesha kufanikisha malengo ya kila upande.

Inapotokea kukwaruzana, ni vema pande hizo zikakaa pamoja na kujadiliana kile kinachosababisha mkwaruzano huo badala ya kuanza kutishana.

Kutoleana vitisho ni njia moja ya kutengeneza woga kwa upande mmoja na hilo si jambo zuri kwa sababu litasababisha upande unaojiona kutishiwa kushindwa kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Kwa kuwa pande hizi zinategemeana, basi upande mmoja ukishindwa kufanya kazi zake kwa ufanisi, athari hazitakuwa kwa upande huo tu, bali hata kwa ule upande mwingine ambao nao unategemea ufanisi wa upande unaotishiwa.

Si vizuri pia pande hizi zikafanya kazi kwa kuviziana kwani hilo litasababisha watumie muda mwingi kutafuta makosa ya mwenzake badala ya kufanya kazi ya kuhimizana kuleta maendeleo na kukosoana kiungwana pale mmoja anapokosea.

Kwa asili, vyombo vya habari vinapaswa kupewa uhuru wa kufanya kazi ili viweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Wapo watawala ambao wanaogopa kuvipa vyombo vya habari uhuru huo kwa kuamini kuwa kufanya hivyo kunaweza kuvipa vyombo hivyo nafasi ya kuiumbua Serikali.

Lakini ukweli ni kuwa Serikali inayofanya kazi zake kwa weledi ni vigumu sana kuaibika kutokana na ripoti za vyombo vya habari kwa sababu hakutakuwa na udhaifu ambao vyombo hivyo vitauripoti.

Mara nyingi, woga wa Serikali kwa vyombo vya habari unatokana na Serikali husika kutotekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Lakini, hakuna jambo zuri kama anapokuwepo mtu ambaye anakuonyesha makosa unayoyafanya kwa sababu hilo linakupa fursa ya kujirekebisha.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Maoni yako hayahaeleweka unakiri kabisa kuwa kama kuna magazeti yanayo eneza upotoshaji na uzandiki siku zote ni hatarisana kwa taifa letu… sasa Mheshimiwa RAIS ameisha liona hilo na u sidhani kaliona peke yake au mara moja yawezekana nimudasasa… na kalipio la MHE RAIS minadhani halimaanishi kuwa anachukia vyombo vya habari na ndiyo maana kuna baadhi amevipongeza nakusema viko balanced wewe kuwa wazi tu mwandishi moyo wako na unachokizungusha havifanani…

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles