30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Magufuli ateta na Balozi mpya wa Marekani

 MWANDISHI WETU– DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amesema Tanzania itaendeleza uhusiano wake mzuri na kati nchi za Marekani na Vietnam

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Dar es Salaam jana, ilisema Rais Dk. Magufuli alipokea hati za utambulisho za mabalozi wawili walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa Tanzania.

Waliowasilisha hati hizo Ikulu, Dar es Salaam ni Dk. Donald Wright aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Marekani hapa nchini na Nguyen Nam Tien, aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Vietnam hapa nchini.

Katika mazungumzo baada ya kupokea hati hizo, Rais Magufuli amewakaribisha mabalozi hao na ameeleza kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yake na nchi hizo.

Mhe. Rais Magufuli amewaomba Mabalozi hao kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini mwao kuja kuwekeza hapa nchini na kwamba Serikali itakuwa tayari wakati wowote kutoa ushirikiano kwao.

Akizungumza baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho,Balozi Wright ameeleza kufurahishwa kwake na kurejea Tanzania baada ya miaka 33 tangu alipokuja kwa mara ya kwanza kufanya kazi za kutoa matibabu.

Alisema tangu wakati huo anawaheshimu na kuwapenda Watanzania kutokana na ukarimu wao, upendo wao na jinsi wanavyoishi na wageni kama wanafamilia wao. 

Alisema Marekani inaiona Tanzania ni nchi imara, tulivu na yenye demokrasia na uhusiano wake mzuri na Marekani umeiwezesha kufanya kazi pamoja na anatarajia kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano zaidi na Serikali ya Tanzania.

Pia Balozi Wright aliwasilisha salamu za rambirambi kwa Rais Magufuli kutoka kwa Rais wa Marekani,Donald Trump na Serikali ya Marekani kutokana na kifo cha Rais mstaafu hayati Benjamin Mkapa na kueleza Marekani inatambua mchango mkubwa wa Mkapa kwa Tanzania na kimataifa.

Naye Nguyen Nam Tien amesema Tanzania ni nchi nzuri, Rais wake anafanya kazi nzuri na anatazamia kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu zaidi ili kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano uliopo.

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi alielezea uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Marekani na kwamba Marekani imekuwa ikifadhili miradi mingi akiwemo afya ambapo imetoa Sh trilioni 1.56 mwaka 2018, miradi 3,179 ya uwekezaji kutoka Marekani ambayo imezalisha ajira 550,000 kwa Watanzania.

Alisema pia mauzo ya bidhaa za Tanzania nchini Marekani yamekuwa yakiongezeka ambapo mwaka jana, bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 119 ziliuzwa nchini humo.

“Uhusiano wa Tanzania na Marekani ni mzuri na unazidi kuimarika na tunaamini kuwa kuja kwa Balozi Wright kutaimarisha zaidi uhusiano huo,” alisema.

Kwa upande wa Vietnam, Profesa Kabudi alisema Tanzania imekuwa na uhusiano wa kidugu na kihistoria na nchi hiyo ambapo inashirikiana nayo katika mambo mengi ikiwemo uwekezaji wa kampuni ya simu za mkononi ya Halotel.

Katika hatua nyingine, taarifa ya ubalozi wa Marekani, ilisema Dk. Wright aliahidi kufanya kazi maeneo makuu manne. “Natarajia kufanya kazi ya kuimarisha uhusiano wetu wa nchi mbili katika nyanja manne ya afya, usalama, utawala na elimu”

Balozi Dk. Wright aliapishwa kama Balozi wa Marekani nchini Tanzania Aprili 2, mwaka huu jijini Washington.

Balozi huyo kwa miaka 17 iliyopita, amekuwa kiongozi sekta ya afya ya umma na sera za afya ngazi za kitaifa na kimataifa. 

“Hii ni pamoja na kuhudumu katika Wizara ya Afya na Huduma za Binadamu ya Marekani, Wizara ya Kazi na Ajira na Umoja wa Mataifa,”ilisema taarifa hiyo. 

Kabla ya uteuzi huo, Balozi Dk.Wright alikuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Huduma za Binadamu.

Taarifa hiyo, hicho ni chombo cha juu kabisa nchini Marekani kinachohusika na masuala ya afya. 

Pia aliongoza Idara ya Kudhibiti Maradhi na Kukuza Afya (Office of Disease Prevention and Health Promotion – ODPHP), Ofisi ya Kusimamia Uadilifu katika Tafiti (Office of Research Integrity – ORI) na Idara ya Usalama wa Afya Kazini (OSHA). 

 Alihudumu kama Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Rais la Michezo, Utimamu wa Kiafya na Lishe (President’s Council on Sports, Fitness and Nutrition – PCSFN.)

Kwa takriban miongo miwili kabla ya kuingia katika utumishi serikalini, Dk. Wright alikuwa daktari akihudumu katika Jimbo alilotokea la Texas, akibobea zaidi katika afya ya familia na usalama wa afya kazini. Katika hafla iliyofanyika hivi leo Ikulu jijini Balozi Dk. Wright anakuwa balozi wa 19 wa Marekani nchini Tanzania. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles