24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

RAIS MAGUFULI ATAJA KILICHOMSHINDA EAC

Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni akigonga nyundo kufungua mkutano wa 18 wa wakuu wa nchi ya jumuiya hiyo, Dar es Salaam jana.Kushoto ni Mwenyekiti wa jumuiya hiyo aliyemaliza muda wake, Rais Dkt John Magufuli.PICHA: SILVAN KIWALE

 

 

NA AZIZA MASOUD -DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amesema katika kipindi cha mwaka mmoja alichoiongoza Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kama Mwenyekiti, ameshindwa kutatua changamoto aliyoikuta ya wanachama kushindwa kusaini mkataba wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ulaya (EPA).

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana wakati wa mkutano wa 18 wa viongozi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo ambao pamoja na mambo mengine alikabidhi uenyekiti kwa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

Alisema ugumu wa kutatua changamoto hiyo ulitokana na kuwapo kwa masharti magumu.

“Nilikabidhiwa uenyekiti nikiwa na miezi minne madarakani, pamoja na mafanikio tuliyoyapa kama jumuiya, pia changamoto zipo.

“Tulitakiwa kusaini mkataba na Umoja wa Ulaya (EU), nikiri katika kipindi changu tulishindwa, wakati wanatuambia tusaini wamewawekea vikwazo Burundi, wao nao wengine kama Uingereza wameshajitoa kwenye umoja wao, nimeliacha bila kulimaliza,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema masharti yaliyopo katika mkataba huo ni mengi na ana uhakika katika kipindi kinachoanza, watazungumza na EU ili waweze kurekebisha masuala ambayo yamewafanya washindwe kusaini.

“Tutazungumza ili tuweze kurekebisha hayo mambo ambayo yalitushinda, lakini lazima na wao wajue kuwa Burundi ni mwanachama wa EAC,” alisema Dk. Magufuli.

Mbali na EPA, alisema changamoto nyingine aliyoshindwa kuitatua na inabidi iendelee kufanyiwa kazi, ni migogoro ya kisiasa iliyopo katika nchi za Sudan Kusini na Burundi.

Aliwataka viongozi wanaovutana katika nchi hizo mbili kuweka masilahi ya mataifa yao mbele na kuacha kuangalia masilahi binafsi ili waweze kutatua migogoro ya kisiasa waliyonayo.

Alisema jumuiya hiyo ilifanya jitihada kuhakikisha inapunguza migogoro hiyo kwa kipindi alichokuwa mwenyekiti.

Pia alisema EAC katika kipindi cha mwaka mmoja imefanikiwa kubana matumizi kutoka Dola milioni 12.6 za Marekani hadi milioni 9.1.

“Tumeweza kufanikiwa kubana matumizi, kwa hizo takwimu utaona tofauti hapo tumeokoa Dola milioni 3.45, najua wapo watu walichukia, lakini tulifanikiwa na Museveni ufanye hivyo hivyo ili fedha ziende kwenye miradi ya maendeleo, hii fedha tukiibadilisha kila mtu katika nchi yake ni fedha nyingi na zimeweza kwenda kufanya maendeleo katika sekta nyingine,” alisema.

Alisisitiza kuwa fedha za EAC zinapaswa kujikita zaidi katika matumizi ya msingi kama utengenezaji wa miundombinu ya nchi husika na si matumizi ya kawaida.

Katika mkutano huo mbali na Museveni ambaye alikabidhiwa uenyekiti marais wengine walituma wawakilishi wakiwamo manaibu rais, makamu wa rais na mawaziri.

Naye Rais Museveni aliitaka EU kuacha kupanga masharti na kuingilia utaratibu wa nchi wanachama wa EAC, kuhusu kusaini mkataba wa EPA kwa kuwa nchi zote zina haki sawa katika makubaliano hayo.

 “Tumekubaliana katika kikao cha ndani   nitaenda Brussels, wasiwaadhibu Kenya na Burundi na kuwaambia Burundi hatutaki EU kuwachukulia hatua mtu yeyote kabla hatujajadiliana,” alisema Museveni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles