28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Magufuli apangua mawaziri

RNa ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri, kwa kuwabadilishia wizara mawaziri wawili.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Mwigwa, ilieleza kwamba katika mabadiliko hayo, Rais Dk. Magufuli amemteua aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Profesa Paramagamba Kabudi.

Pamoja na hilo, pia mkuu huyo wa nchi amemteua aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa  Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Balozi Mahiga.

Taarifa hiyo ya Ikulu ilieleza kwamba, mawaziri hao wateule wataapishwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam saa 3:30 asubuhi. 

Hatua hiyo ya Rais Dk. Magufuli kulifanyia mabadiliko madogo baraza lake la mawaziri imeendelea kuzua maswali mengi, kwa kuwa mawaziri aliowateua katika nyadhifa mpya walikuwa wachapakazi katika wizara zao za awali.

Kutokana na uteuzi huo, baadhi ya wanasiasa na wafuatiliaji wa masuala ya siasa nchini, wametoa maoni yao kuhusu uteuzi huo huo ambapo Profesa Kabudi ambaye kitaaluma ni mtaalamu wa sheria na Balozi Dk. Mahiga ambaye kitaaluma ni mtaalamu wa diplomasia.

Wote wawili ni wabunge wa kuteuliwa na rais ambao walipata uteuzi kwa nyakati tofauti, baada ya Rais Dk. Magufuli kuingia madarakani Oktoba mwaka 2015.

Tangu kuteuliwa kwake, Prof Kabudi ambaye amewahi kuwa mwalimu wa sheria chuo kikuu, anaonekana ni mtetezi mahiri wa sera za Serikali ya Rais Dk. Magufuli. 

Katika maoni yake kupitia ukurasa wake wa Twitter, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na Mbunge wa Kigoma, Zitto Kabwe, aliandika: “Mabadiliko hayo ni hatua kubwa kwa Tanzania kuelekea kutiwa saini kwa mkataba wa kibiashara kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya na hali kadhalika kutolewa kwa nafasi ya mashauriano ya kisiasa.”

Kabudi pia ameongoza mazungumzo kati ya Serikali na wawekezaji wakubwa wa nje kama Barrick Gold Corp na Bharti Airtel ya India, ambapo kampuni hiyo ilikubali kurejesha hisa zake kwa Serikali.

Kutokana na hilo, inatarajiwa kama Waziri mpya wa Mambo ya Nje, ataweza kuisaidia Tanzania kupata maelewano zaidi na nchi wafadhili. 

Katika hatua nyingine, Kabudi alionyesha umahiri wa hali ya juu alipokuwa akizungumza na Jumuiya ya Watanzania waishio nchini Canada alipokutana nao mjini Seatle, ikiwa ni hatua ya kunadi juhudi zinazofanywa na Serikali ya Rais Dk. Magufuli. 

Pamoja na hali hiyo, pia Balozi Dk. Mahiga anatajwa kama mwanadiplomasia mbobezi ambaye kwa mara kadhaa alikuwa akienda nje ya mipaka ya Tanzania kumwakilisha Rais Dk. Magufuli katika shughuli mbalimbali.

Pamoja na hali hiyo, amekuwa akitumia taaluma yake kuelezea sifa nzuri ya Tanzania kwa nchi rafiki wa maendeleo kwa Tanzania, huku akizihakikishia usalama na kukua kwa demokrasia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles