FLORIAN MASINDE , DAR ES SAALAM
RAIS John Magufuli jana aliongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa Leticia Nyerere nyumbani kwa familia ya hayati Mwalimu   Nyerere, Msasani  Dar es Salaam.
Rais  aliwasili nyumbani hapo akiongozana na mkewe Janeth na moja kwa moja alikwenda kusaini kitabu cha maombolezo.
Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sifue, marais na mawaziri wakuu wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Jakaya Kikwete, Mizengo Pinda   na Spika mstaafu,   Anna Makinda.
Mwili wa Leticia aliyefariki dunia  Marekani alikokuwa amelazwa uliwasili juzi saa 9 alasiri na kupokewa na ndugu, jamaa na marafiki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Baadaye ulipelekwa katika Kanisa la Mtakatifu Peter kwa ajili ya Ibada   na neno la faraja kwa familia.
Viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Rais mstaafu, Benjamin Mkapa waliongoza waombolezaji katika ibada hiyo. Wengine waliohudhuria ibada hiyo maalum ni Spika mstaafu, Anna Makinda na Jaji Joseph Warioba.
Jana mwili wa marehemu Leticia ulisafirishwa kupelekwa kijijini Butiama kwa mazishi.
Leticia ambaye ni mtoto wa mwanasiasa mkongwe, Musobi Mageni alizaliwa wilayani Kwimba mkoani Mwanza 1954 na kupata elimu yake ndani na nje ya Tanzania kwa vipindi tofauti.
Marehemu Leticia ambaye ni mtalaka wa mtoto wa baba wa taifa, Madaraka Nyerere ameacha watoto watatu.