*Awatangazia kiama viongozi wanaotafuna mali za chama
*Aagiza Takukuru kumchunguza Kisena wa UDA
Na Waandishi Wetu, Mwanza/Dar
RAIS Dk. John Magufuli, sasa amegeukia utumbuaji majipu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akituma salamu kwa viongozi wa chama hicho ngazi ya taifa, mikoa, wilaya, kata na matawi.
Kutokana na hali hiyo, amesema hivi sasa mafisadi ndani ya CCM hawana nafasi na anataka kukirudiusha chama hicho kwenye misingi ya uadilifu na nidhamu, kama ilivyokuwa enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini Mwanza, alipokuwa akihutubia mamia ya wananchi katika Uwanja wa Furahisha, ambapo alisema ili kuhakikisha nidhamu inarudi ndani ya CCM mali zote za chama hicho zitakaguliwa ili mapato yake yaweze kujulikana na si kuwaachia viongozi wachache ambao wamekuwa wakizitumia kwa masilahi yao binafsi.
Rais Magufuli, alisema hawezi kuhamasisha wananchi wawe na nidhamu wakati chama chake hakina nidhamu jambo ambalo atahakikisha analirudisha kwa nguvu zake.
“Napenda niongoze chama ambacho mali na majengo yake yanajulikana na si kuongoza chama ambacho haujui kinaingiza mapato kiasi gani, lazima ifike mahali turudishe hadhi ya chama kama ilivyokuwa enzi za Mwalimu Nyerere na si kuwaachia watu wachache wagawane fedha za chama.
“Mafisadi hawako ngazi za chini ila wapo katika ngazi za mikoa na taifa sasa nawaambia wajiandae. Naomba niseme kuwa, mafisadi hawana nafasi ndani ya CCM… tayari wameshaanza kuondoka.
“…. waache waende na wakirudi watakuwa wamekatika mikia, siwataki watu ambao mchana wapo CCM na usiku wanahamia chama kingine, waondoke tu ni bora tubaki wachache ambao ni waadilifu ili tuendelee kutawala kwa sababu Watanzania wanahitaji maendeleo na si vyama,” alisema Magufuli.
Alisema analazimika kuchukua hatua hiyo ndani ya chama baada ya kuonekana mafanikio ndani ya Serikali ambayo kwa sasa imedhamiria kurudisha nidhamu kwa viongozi.
“Hizi fedha za majengo ya chama zingekuwa zinakusanywa, wanachama mngeweza kugawana walau mara mojamoja…, bahati nzuri nimekuwa mwenyekiti sasa ni lazima wanachama muanze kuhoji kwenye vikao vyenu haya mapato na wakiwauliza nani anawapa jeuri ya kuwahoji waambieni mwenyekiti,” alisema.
Alisema CCM Mkoa wa Mwanza inalo jengo la ghorofa sita ambalo limepangishwa maduka makubwa lakini ukiuliza gharama za upangishaji huwezi kupata gharama sahihi kwa kuwa wamekuwa wakiandika Sh 50,000 na wakati mwingine gharama halisi ni Sh 300,000.
Alisema lazima wasimamie mali za chama na kuonya kuwa chini ya uongozi wake kamwe viongozi watakaowania nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa chama watakaobainika kutoa rushwa atawakata majina yao ili kuwaengua kugombea.
Kutokana na hali hiyo alisema mafisadi wakae chonjo kwani atawatia mbaroni na kuwafikisha kwenye mikono ya sheria ili rasilimali za Watanzania ziendelee kudumu.
Alisema hadi sasa Serikali imetenga Sh bilioni 1.2 kwa ajili ya kuanzisha Mahakama ya Mafisadi ambayo itawachukulia hatua watendaji wote watakaobainika kutumia fedha za umma vibaya.
Alisema, kutokana na hali hiyo, viongozi wanapaswa kufanya kazi na kuwachukulia hatua wale watakaobainika kwenda kinyume na majukumu yao na kwamba watakaobainika wanataka kuwakwamisha, wawachukulie hatua ili waweze kukwama wenyewe.
Rungu kwa Polisi
Alisema hadi sasa Jeshi la Polisi limeweza kutimiza majukumu yake ipasavyo hasa katika uamuzi wa kupambana na majambazi.
“Kazi mliofanya ya kupambana na majambazi wale ni kubwa, nawasisitiza anayetaka kuchezea moto muwasheni hapo hapo…tumechoka kubembelezana lazima watu wafanyekazi na si ujambazi,” alisema.
MACHINGA
Akizungumzia kuhusu wamachinga, Rais Magufuli aliwaagiza viongozi wa Mkoa wa Mwanza kuacha kuwaondoa wamachinga katikati ya Jiji na kuwataka kukaa nao ndani ya kipindi cha miezi miwili au mitatu ili waweze kuangalia sehemu nzuri ya kuwapeleka kwa ajili ya kufanya shughuli zao.
“Huwezi kuwapeleka wamachinga mlimani, wanakwenda kumuuzia nani? Hawa ndiyo walionichagua mimi, ninaomba muwaache hapo halafu mkae na kujadiliana nao ndani ya miezi miwili au mitatu ili mjue wapi wataweza kwenda kufanya shughuli zao ili waweze kupata faida kwa sababu na wenyewe wanatafuta pesa,” alisema.
Aliongeza, lakini wamachinga wanapaswa kutambua kuwa, Serikali inataka kodi, hivyo basi wasikubali kutumiwa na wafanyabiashara wakubwa ambao ndiyo wakwepa kodi kwa kuwapa bidhaa bila ya stakabadhi hali inayoweza kusababisha kukamatwa.
“Mkienda kununua bidhaa lazima wawape risiti ya EFD, kwa sababu wafanyabiashara wamekuwa na tabia ya kuwapa bidhaa zao na kwenda kuuza huku wakijua kuwa wanakwepa kodi,” alisema.
Simon Group kuchunguzwa
Kiongozi huyo wa nchi alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. CharlesTizeba pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuzirejesha mali za Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU LTD) kikiwemo Kiwanda cha New Era kilichouzwa kwa Kampuni ya Simon Group inayomilikiwa na Simon Kisena.
Simon Group chini ya mwenyekiti wake mtendaji, Simon Kisena ndiyo walipewa tenda ya kuendesha Shirika la Usafiri Jiji la Dar es Salaam (UDA), ambapo suala hilo bado giza nene limetanda.
Hatua hiyo ilimfanya Rais Magufuli, kusema kuwa NCU iliwahi kutangazwa kuwa miongoni mwa vyama vikubwa vya ushirika barani Afrika kutokana na kufanya vizuri, lakini sasa iko hoi huku mali zake zilizoenea kila sehemu zikiwemo Ginnery zikiuzwa kwa bei ya kutupa.
Kutokana na hali hiyo aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru), vyombo vya ulinzi na usalama kuanza uchunguzi haraka ili mali hizo za NCU zilizouzwa zirejeshwe huku akikitaja kiwanda cha New Era ambacho alisema kimeuzwa kwa Simon Kisena wa Kampuni ya Simon Group Ltd nacho kirejeshwe.
“Ninaifahamu Nyanza maana mimi nimefanya kazi New Era, sasa imeuzwa kwa Shilingi milioni 32 badala ya Sh bilioni 1, vyombo vya usalama vipi, Takukuru ipo sasa sijui mnachunguza nini kama siyo haya, mali zipo nataka zirejeshwe kwa wakulima.
“Najua aliyeuziwa ni Simon Group, mimi huwa sifichi sasa nataka mlisimamie hili na hizo mali zirejeshwe kwa wakulima kama ulivyoeleza Mkuu wa Mkoa,” alisema Rais Magufuli.
Pamoja na hali hiyo alimtaka Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, kusimamia jambo hilo huku akimuonya kutoogopa kupoteza kura wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwani yeye kama Rais anavyo viti vya ubunge na atamteua tena kushika nafasi hiyo.
Uvuvi haramu
Rais Magufuli amemuagiza Waziri Tizeba kuanzisha oparesheni ya kusaka nyavu haramu na makokoro kwa kuyachoma moto ili kuliokoa Ziwa Victoria kwa faida ya kizazi kijacho.
Alisema kabla ya kuwa rais aliwahi kuwa Waziri wa Uvuvi na kwamba alichoma moto na kuteketeza makokoro hivyo kumtaka kuanzisha oparesheni ndani ya Ziwa Victoria ikiwa ni pamoja na kukamata magari yanayosafirisha nyavu haramu ikiwa ni pamoja na kutaifisha magari yanayozisafirisha kuziingi hapa nchini.
Utekelezaji wa ahadi
Akizungumzia ahadi alizotoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alisema alihaidi kutoa elimu bure na kwamba mara baada ya kushinda aliamua kusaka fedha za kukamilisha mpango wake kwa kuanza kusimamia ukusanyaji wa mapato bandarini ambako alifanikiwa kukusanya mabilioni na kuanza mfumo wa utoaji elimu bure.
Alisema katika bajeti ya mwaka huu serikali yake imetenga fedha Sh trilioni moja za kununulia meli moja mpya ya kubeba abiria 1000 na tani 400 za mizigo itakayotoa huduma Ziwa Victoria na ikiwa ni pamoja na kuanza ujenzi wa reli ya kiwango cha Standard Gage.
Alisema pia kutokana na kubana matumizi na kuzuwia safari za nje ya nchi kwa watumishi wa Serikali ameweza kupata fedha za kununulia ndege mbili nchini Canada ambapo kwa sasa zinatarajia kuwasili mwezi Septemba mwaka huu na kuanza kutoa huduma huku ndege nyingine ikiendelea kutengenezwa.
Hata hivyo aliagiza mkandarasi anayeshughulika na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza kuendelea mara moja ili uwanja huo ukamilike na kuwa wa kisasi utakaotoa huduma ya ndege kubwa hivyo kuufanya mji wa mwanza kuwa kitovu cha nchi za maziwa makuu.
Mongela
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema katika moja ya mipango yake Mkoa wa Mwanza amedhamiria kufufua kilimo cha zao la pamba ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanarejesha mali za Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza ambazo ziliuzwa kwa bei ya kutupa.
Mongella alisema NCU waliuza majengo yake manne likiwemo la jengo la makao makuu ya chama hicho pamoja na hosteli za Pamba huku akibainisha kuwa kiwanda cha New Era kiliuzwa kwa Sh milioni 32 pamoja na uuzwaji wa viwanja vinne kwa Sh milioni 70 vyote vikiwa ni mali ya ushirika.
Mongella, alisema NCU imeliwa na sasa wameanza kusimamia urejeshaji wa mali zake kwa kushirikiana Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. CharlesTizeba na kuomba awaunge mkono ili kuhakikisha mali hizo zinarejea na ushirika unakuwa na hadhi yake.
Habari hii imeandaliwa na Judith Nyange na Peter Fabian (Mwanza), Patricia Kimeleta na Veronica Romwald (Dar es Salaam)