NA OSCAR ASSENGA, TANGA
RAIS Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwasili mkoani Tanga leo kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku nne mkoani hapa itakayoambana na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya nne atakazotembelea.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga jana, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Luteni mstaafu Chiku Gallawa, alisema katika ziara hiyo, Rais Kikwete atapokelewa Kijiji cha Kimbe wilayani Kilindi.
Wilaya zinazotarajiwa kutembelewa na Rais Kikwete ambazo katika awamu ya kwanza hakuzitembelea ni Lushoto, Kilindi, Mkinga na Pangani.
Gallawa aliitaja miradi itakayozinduliwa na Rais Kikwete kwamba katika Wilaya ya Lushoto atafungua jengo la kisasa la wafugaji wa nyuki na kutoa vifaa vya kilimo, ikiwemo kugawa matrekta.
Alisema kwa Wilaya ya Mkinga, Rais Kikwete atakagua nyumba zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa Tanzania (NHC) na nyumba za watumishi.
Gallawa alisema nyumba hizo za NHC za bei nafuu zitakuwa ni za watumishi, kwa sababu Wilaya ya Mkinga ina upungufu mkubwa wa nyumba za watumishi.
“Nyumba hizo zilijengwa na Shirika hilo la Taifa la Nyumba kwa thamani ya Sh bilioni 1.2 kwa nyumba zipatazo 40 kwenye wilaya hiyo, wakiwa na lengo zinunuliwe na halmashauri hiyo ili kuweza kuondoa uhaba wa nyumba za watumishi wilaya hii,” alisema.
“Napenda kutoa wito wananchi kwenye maeneo mbalimbali atakapopita wajitokeza kwa wingi kumlaki Rais Kikwete, ambaye atakuwa akipita kwenye barabara mbalimbali wilayani humo,” alisema Gallawa.