23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Kiir atekeleza takwa la upinzani

Juba, Sudan Kusini

AFRIKA Kusini imepongeza hatua ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ya kupunguza idadi ya majimbo nchini humo, moja ya matakwa makuu ya upinzani unaoongozwa na Riek Machar, kwa ajili ya kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

David Mabuza, Makamu wa Rais wa Afrika Kusini ambaye pia ni mjumbe maalumu wa Sudan Kusini jana alisema kuwa, “hatua ya kimapinduzi iliyochukuliwa na Rais Salva Kiir imeandaa mazingira ya kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kabla ya kumalizika muda ulioanishwa unaomalizika ndani ya wiki moja.” 

Rais Kiir amepunguza idadi ya majimbo ya nchi hiyo changa zaidi barani Afrika kutoka 32 hadi 10. Akizungumzia uamuzi huo juzi Jumamosi, Kiir alisema “uamuzi tuliochukua ni wenye kuumiza lakini wa lazima iwapo utaleta amani.”  

Kiir aliongeza idadi ya majimbo ya nchi hiyo iliyojipatia uhuru wake 2011 kutoka 10 hadi 28 mwaka 2015 na kisha hadi 32 baadaye, wakati mgogoro na vita vya ndani nchini humo ulipokuwa umeshika kasi.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.

Mwaka jana, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na Riek Machar, kiongozi wa waasi, walikubaliana kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya vuta nikuvute ya muda mrefu. Februari 22 ndio tarehe ya mwisho iliyoainishwa kwa ajili ya kuundwa Serikali hiyo.

Umoja wa Afrika (AU) umeelezea kufurahishwa kwake na juhudi za kuutafutia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa Sudan Kusini ambao unalenga kurejesha amani katika nchi hiyo iliyokumbwa na machafuko tangu kuasisiwa kwake.

Hata hivyo, waasi wa Sudan Kusini wamelikataa pendekezo la amani la Rais Kiir, kurejesha mfumo wa majimbo 10, ili kufungua njia ya kuundwa kwa Serikali ya umoja wa kitaifa ya taifa hilo.

Hatua hiyo ya kiongozi wa waasi Riek Machar inaondosha matumani ya kuumaliza mkwamo na kuhitimisha mgogoro wa miaka sita uliosababisha vifo vya watu wasiopungua 380,000 na kuwaacha mamilioni katika hali mbaya ya umaskini.

Kiir na Machar wapo katika shinikizo kubwa la jumuiya ya kimataifa kumaliza tofauti zao kufikia muda wa mwisho wa Februari 22 mwaka huu.

Juzi, Kiir alisema taifa hilo kwa sasa litagawanywa katika majimbo 10, likiwa takwa muhimu la upinzani, pamoja na maeneo matatu ya kiutawala ambayo ni Pibor, Ruweng na Abyei.

Lakini kiongozi wa waasi Riek Machar alisema jana kuwa anapinga maeneo hayo matatu ya kiutawala.

Katika taarifa yake, Machar alisema hatua hiyo haiwezi kutajwa kama kurejesha mfumo wa majimbo 10 na kuonya hilo linaweza kusababisha matatizo zaidi.

Idadi ya majimbo inasababisha ubishani kwa sababu mipaka itaamua mgawanyiko wa madaraka katika taifa hilo tete.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles