RAIS KENYATTA, JAJI MKUU WASHAMBULIANA

0
467

NAIROBI, KENYAJAJI Mkuu wa Kenya amemuonya Rais Uhuru Kenyatta kutoathiri imani iliyopo kwa mfumo wa mahakama, katika mashambulizi yasiyo ya kawaida baina ya wawili hao, ikiwa umebaki chini ya mwezi mmoja kabla ya chaguzi kufanyika.

Awali Kenyatta akikasirishwa na ushindi wa upinzani dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), alionya dhidi ya jaribio lolote la kutumia mchakato wa mahakama kuchelewesha chaguzi.
“Wanatuchukulia wajinga, aliuambia mkutano wa hadhara katika kaunti ya Baringo, akimaanisha mfumo wa mahakama.

“Nataka kuwaambia walio mahakamani, tumewaheshimu. Lakini msifikirie heshima katika woga. Na hatutaruhusu wapinzani wetu kutumia mahakama kuikwamisha na kuitisha IEBC, wakidhani watashinda kwa kutumia mlango wa nyuma,” alisema.

Jaji Mkuu David Maraga alitoa taarifa saa chache baadaye akisema: “Wakati viongozi wa kisiasa wanapoingilia maamuzi ya mahakama yanayotolewa kwa misingi ya sheria, ina uwezekano mkubwa wa kuathiri imani ya umma kwa mahakama zetu na hili linanisikitisha.”

Upinzani umefungua kasi kadhaa dhidi ya IEBC ikiwamo moja iliyotolewa uamuzi Ijumaa iliyopita, ambayo iliungana nao kwamba mkataba wa kuchapisha karatasi za kura za urais haukutolewa kwa uwazi.

Wakati huo huo, Tume ya Mishahara na Marupurupu ya Watumishi wa Umma nchini Kenya (SRC), imetangaza kupunguzwa kwa mishahara ya maafisa wakuu wakiwemo rais na wabunge.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Sarah Serem ametoa mpangilio mpya wa malipo, ambao amesema utaokoa Sh bilioni 8 za Kenya sawa na Sh bilioni 160 za Tanzania kila mwaka na kupunguza jumla ya mishahara inayolipwa watumishi wa umma kwa asilimia 35 .

Rais sasa atakuwa akilipwa Sh milioni 28 za Tanzania kila mwezi badala ya Sh milioni 33 huku naibu wake akilipwa Sh milioni 24 za Tanzania.

Mawaziri watakuwa wakilipwa Sh milioni 18 za Tanzania, Spika wa Bunge Sh milioni 22 magavana wa kaunti Sh milioni 18.

Mabadiliko hayo yataanza kutekelezwa Agosti, 8 2017.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here