27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

‘Rais Kabila kuwania urais 2023’

KINSHASA, DRC

WAKATI Umoja wa Ulaya (EU ukirefusha muda wa vikwazo mgombea urais wa muungano unaotawala hapa, Rais Joseph Kabila amedokeza kuwa hajafutilia mbali uwezekano wa kuwania tena urais wakati wa uchaguzi wa mwaka 2023.

Amesema ataendelea kuwapo katika siasa hata atakapoondoka madarakani baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika wiki mbilizijazo.

Hayo yanajiri huku EU ukitangaza kuwa umeongeza muda wa kutekelezwa kwa vikwazo dhidi ya watu 14 mashuhuri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hadi Desemba mwaka ujao.

Miongoni mwa wanaoathiriwa na vikwazo hivyo ni mgombea wa muungano wa Kabila, Emmanuel Ramazani Shadary.

Watu hao wamewekewa vikwazo vya kuzuiwa kwa mali yao na pia kupigwa marufuku ya kuingia EU kutokana na hujuma zao katika mchakato wa uchaguzi nchini DRC na ukiukaji wa haki za binadamu.

Kabila alitarajiwa kuondoka madarakani miaka miwili iliyopita baada ya kuongoza kwa mihula miwili kwa mujibu wa katiba.

Hata hivyo, uchaguzi mkuu nchini humo uliahirishwa mara kadhaa, serikali ikisema maandalizi hayakuwa yamekamilika vyema.

Upinzani ulichukulia hilo kama njama ya Kabila kutaka kuendelea kuongoza.

Agosti mwaka huu, Kabila alimtangaza mshirika wake wa karibu Emmanuel Ramazani Shadary ambaye ni waziri wa zamani wa mambo ya ndani kuwa mgombea wa muungano wa kisiasa unaotawala kwa sasa.

Katibu wa chama cha upinzani cha Movement for the Liberation of Congo (MLC), Eve Bazaiba, amesema Shadary atadhibitiwa na Kabila na kwamba kimsingi itakuwa ndiye anayeongoza nchi.

“Anataka tu kusalia madarakani. Hata kama alimchagua Shadary, Shadary ni mtu tu wa kuonekana, ndiye atakayemuongoza Shadary kwa kila jambo. Kiuhalisia, atakuwa bado ndiye rais,” alisema.

Kwa muda mrefu, ilikuwa bado haijabainika iwapo Rais Kabila, angewania tena hadi alipoamua kumtangaza Shadary kuwa mgombea wa muungano wake wa kisiasa.

Kwenye mahojiano na Shirika la Habari la Reuters, Rais Kabila alisema “kwanini tusisubiri hadi mwaka 2023, ndiyo tuweke wazi mambo haya?.”

“Maishani sawa na ilivyo katika siasa, hauwezi kufutilia mbali uwezekano wa jambo kama hilo,” alisema.

Lakini pia kumekuwa na wasiwasi kutoka kwa upinzani na jamii ya kimataifa kuhusu iwapo uchaguzi wa DRC utakuwa huru na wa haki, kitu ambacho Kabila amedai hakina msingi.

Kabila aliingia madarakani akiwa na miaka 29 baada ya kuuawa kwa baba yake Laurent Desire Kabila mwaka 2001.

Aliahidi kurejesha amani na kutokomeza ufisadi na amekuwa akitaja hayo kama baadhi ya mafanikio ya utawala wake.

Kabila amesema anataka kusalia katika siasa ili kulinda mafanikio hayo na kuongeza kuwa wanaotaka kutoa uamuzi kuhusu mafanikio yake wanaweza kusubiri hadi amalize kazi yake.

“Bado kuna safari ndefu mbele yetu na kuna sura nyingi, ambazo zitaandikwa kabla ya kuanza kuandika vitabu vya historia.”

Katiba nchini DRC inamzuia mtu aliyeongoza kwa mihula miwili mfululizo kuwania tena urais, lakini haijazuia mtu kama huyo kuwania tena baada ya kiongozi mwingine kuingia madarakani.

Baadhi wanasema huenda kikawa kisa kama cha Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye baada ya kuongoza kama rais kati ya 2000 na 2008, alikuwa waziri mkuu kati ya 2008 na 2012 kabla ya kurejea tena kuwa rais wa nchi hiyo.

Alibadilishana na mwandani wake Dmitry Medvedev ambaye kwa sasa ndiye waziri mkuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles