29.7 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Erdogan Uturuki azidi kufichua mauaji ya mwandishi

MAUAJI ya kinyama dhidi ya mwandishi wa habari, Jamal Khashoggi yalipangwa na kikosi cha mauaji cha Saudi Arabia, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameliambia Bunge la nchi yake jana.

Wakati Erdogan akitaka kufahamu aliyeamuru mauaji hayo, akikwepa kumtaja Mwana Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, ushahidi mpya unadaiwa kuzidi kumnyooshea kidole kiongozi huyo mwenye nguvu Saudi Arabia.

Vilevile, wakati Erdogan katika hotuba yake hiyo akitaka pia kuonyeshwa yaliko mabaki ya mwili wa mwandishi huyo, taarifa nyingine  ambayo bado haijathibitisha, inadai yamepatikana katika makazi ya balozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul ukiwamo uso uliochunwa.

Alichozungumza Erdogan

Katika hotuba iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu lakini akaishia kutoa taarifa ambazo tayari zilishavujishwa na vyanzo mbalimbali vya habari vilivyoomba kuhifadhiwa, Erdogan alisema kuna ushahidi wa wazi kuwa kikundi cha wauaji kutoka  Saudi Arabia kilipanga kumuua mwandishi huyo mkosoaji wa ufalme huo kabla ya Oktoba 2 mwaka huu.

Erdogan (64) ameeleza mauaji hayo kuwa ya siasa lakini alisita kumlaumu moja kwa moja Mohammed bin Salman maarufu kama MBS, badala yake ametaka kumfahamu aliyeagiza kufanyika kwa operesheni hiyo.

Alisema alikuwa na matumaini ya kupata ushirikiano kamilifu kutoka kwa Mfalme Salman, baba wa MBS.

“Saudi Arabia imechukua hatua muhimu ya kukiri mauaji. Kwa sasa tunatarajia wale walioshiriki kuanzia ngazi ya juu hadi chini watafikishwa mahakamani,” alisema.

Maofisa wakiwamo wa inteljensia, usalama na alama za vidole, walionekana wakiingia katika jingo ambalo Khashoggi alitoweka huku wengine wakiwa wameonekana wakikagua  msitu wa karibu najengo hilo kabla ya mauaji kutokea, alisema Rais Erdogan.

Ufichuajii huo wa Rais utachochea minong’ono kuwa kikundi hicho kilikuwa kikitafuta eneo ambalo kilipanga kuuzika mwili wa Khashoggi.

Erdogan ametaka watu 18 waliokamatwa na Saudi Arabia kuhusiana na mauaji hayo washitakiwe   Istanbul na kwamba kuwatupia lawama baadhi ya maofisa wa inteljensia kwa mauaji hayo hakutairidhisha Uturuki wala jamii ya mataifa.

Akizungumza na wanachama wa Chama chake cha AK Bungeni, Erdogan, ambaye binafsi amekuwa akishutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu, alihoji kwa nini mwili wa Khashoggi haujapatikana.

Aliitaka Saudi Arabia kumfichua mtu aliyepewa jukumu la kuupoteza mwili huo, ambaye inaaminika ni Mturuki.

Sehemu ya mabaki yagundulika

Wakati Erdogan akitaka kufahamu ulipo mwili huo, kuna taarifa kuwa uligundulika katika bustani ya balozi mdogo wa taifa hilo, kwa mujibu wa ripoti za Sky News jana, lakini haikufahamika ukubwa wa sehemu iliyogundulika.

Ripoti tofauti zinasema sehemu ya mwili huo ilikutwa katika kisima.

Iwapo itathibitishwa ni kweli, maswali yataibuka kuhusu sababu ya kupita muda mrefu kugundua yalipo mabaki ya mwili wa Khashoggi.

Balozi Mdogo wa Saudi Aarabia, Mohammed al-Otaibi alikimbia Istanbul wiki iliyopita kabla ya nyumba yake hiyo kukaguliwa na polisi wa Uturuki.

Nchini mwake, amewekwa chini ya uchunguzi na kuondolewa cheo chake, ufalme ulisema katika taarifa .

Mapema jana, Erdogan alisema alimwambia Mfalme Salman kuwa balozi huyo hafai kwa kazi hiyo.

Erdogan alizungumza kwa simu mara mbili na Mfalme Salman, kitu kinachotafsiriwa na wengi kama mkakati wa kumweka pembeni Prince Mohammed ambaye baba yake amezeeka.

Ingawa   masuala aliyozungumza  tayari yalishavuja, lakini kwa Erdogan kutoa hotuba Bungeni kunayapa nguvu madai hayo.

Mmoja wa wanadiplomasa wa Magharibi nchini Uturuki ameuambia mtandao wa Bloomberg kwamba mgogoro huo ni ‘zawadi kutoka kwa Mungu’ kwa Erdogan wakati akijaribu kujijenga kuleta mabadiliko ya uwiano wa nguvu nchini Saudi Arabia na kuongeza ushawishi wake Mashariki ya Kati.

“Kwa nini watu hawa 15 wakutane  Istanbul   siku ya mauaji? Tunatafuta majibu  ya swali hili. Watu hawa walikuwa wakipokea amri kutoka kwa nani?” Erdogan alisema.

“NInachotaka ni kwamba watu hawa 18 washitakiwe Istanbul,” Erdogan alisema katika hotuba yake, akizungumzia   watu hao wakiwamo maofisa wa usalama ambao tayari wamekamatwa mjini Riyadh.

Alisema wote walioshiriki katika mauaji hayo wanapaswa kukabiliwa na adhabu kali.

Erdogan alisema  mauaji yanaonekana yalipangwa kulingana na ramani iliyoandaliwa na kikundi cha  Saudi Arabia, ambayo ilitumwa Istanbul kwa madhumuni hayo.

Mfumo wa usalama katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia ulizimwa kwa makusudi kwa   madhumuni hayo, alisema.

“Haya ni mauaji ya siasa,” Erdogan alisema.

Simu saba zapigwa Ofisi ya Mwana Mrithi wa Ufalme

Pamoja na kutomtaja Mohamed, ushahidi unaelekezwa huko kwa vile idadi  kubwa ya watu hao 15 walioingia Istanbul wanamfanyia kazi.

Mmoja wao, Meja Jenerali  Maher Abdulaziz Mutrib, mwanadiplomasia wa zamani, anadaiwa alipiga simu 14 kwenda Saudi Arabia zikiwamo saba kwenda kwa Ofisi ya Muhammad baada ya Khashoggi kuuawa.

Simu hizo zilinaswa na vyombo vya usalama vya Uturuki, maudhui ambayo yanahatarisha hatima ya baadaye ya siasa ya MBS  iwapo yatavujishwa, kwa mujibu wa chanzo cha habari.

Mutrib, ambaye amekuwa akisafiri katika ziara karibu zote za Salman, ameelezwa kuwa uti wa mgongo wa kikosi cha mauaji cha Saudi Arabia.

Tuhuma hizo ni mwendelezo mwingine unaoelekeza kidole kwa mtawala huyo wa Saudi Arabia mwenye nguvu.

MBS adaiwa aliapa kuwakata vidole wakosoaji

Wakati Saudia Arabia ikitupia lawama kwa maofisa wengine kwa kumuua Khashoggi (59) kwa utashi wao, chanzo cha habari cha kuaminika kilisema kikosi hicho cha siri kilituma vidole vya Khashoggi mjini Riyadh  kuthibitisha kuwa operesheni hiyo ilifanikiwa na viliwasilishwa kwa MBS.

“MBS daima hupanda kusema atakata vidole vya kila mwandishi anayemkosoa,” chanzo hicho kilidai.

Kwa mujibu wa gazeti la Yeni Safak, Mutrib alizungumza na Badr al-Asaker, mkuu wa ofisi binafsi ya Mwana Mrithi wa Ufalme, mara nne baada ya Khashoggi kuuawa.

Vyanzo vya habari vya Saudia na Uturuki vilisema utawala wa kifalme umemfukuza msaidizi mmoja kwa kuamuru mauaji kupitia mtandao wa video wa Skype.

Saud Al-Qahtani, ambaye anasimamia mtandao wa jamii maalumu kwa Mwana Mrithi Ufalme, anadaiwa kumtukana mwandishi huyo baada ya kukamatwa katika ubalozi huo akikiambia kikosi hicho, ‘nileteeni kichwa cha mbwa huyo.’

Alifukuzwa wadhifa wake na kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa Shirikisho la Usalama wa Mitandao, Programu na Drone, wadhifa alioukuwa nao awali.

Kashfa hiyo imeathiri mkutano wa Jukwaa la Uwekezaji Saudi lililofunguliwa jana baada ya makampuni makubwa ya kimataifa kujitoa.

Mradi huo ni ubunifu wa Mwana Mrithi wa Ufalme Mohammed bin Salman, ukilenga kuvutia uwekezaji zaidi wa kigeni kaika ufalme huo na kusaidia kutengeneza ajira kwa   vijana wengi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles