RAIS ERDOGAN AAPA KUWAKATA VICHWA WAASI

0
564

ANKARA, UTURUKI


RAIS Recep Tayyip Erdogan juzi aliapa kuwa atawakata vichwa wafuasi wa makundi ya kigaidi na wale wote waliopanga njama za kuupindua utawala wake uliodumu kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Erdogan ametoa kauli hiyo wakati Uturuki ikiadhimisha mwaka mmoja tangu kufanyika jaribio la mapinduzi lililoshindwa Julai 15 mwaka jana.

Akiongozana na familia yake pamoja na ndugu wa waathirika wa jaribio hilo, Rais Erdogan aliungana na umati uliokuwa ukipepeperusha bendera mjini Istanbul kuwakumbuka watu 250 waliouawa katika tukio hilo wakipinga mapinduzi.

Alisema jaribio la mapinduzi la Julai mwaka jana si shambulizi la kwanza dhidi ya serikali na kwa vile halitakuwa la mwisho, serikali yake italazimika kuwakata vichwa wale wote, ambao ni wasaliti.

Aidha Rais Erdogan alizindua sanamu ya kumbukumbu iliyo na majina ya waathirika wa jaribio hilo kabla ya kusafiri kwenda mjini Ankara kushiriki kikao maalumu cha Bunge.

Kikao hicho kilifanyika muda ule ule, ambao mashambulizi ya mabomu dhidi ya Bunge yalifanyika mwaka jana.

Aidha akihudhuria mkutano uliohudhuriwa na makumi kwa maelfu ya watu mjini hapa jana, Erdogan aliwasifu wafuasi wake waliozima jaribio hilo.

Maadhimisho hayo yanajumuisha pia sauti na video za shambulio lililotokea, kwenye majengo ya Bunge, ambalo lilitekelezwa na vikosi vya waasi.

Hata hivyo, wapinzani wa Erdogan, ambaye anashutumiwa kwa kutumia jaribio hilo la mapinduzi kuwakandamiza wapinzani wake, hawakuhudhuria maadhimisho hayo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here