RAIS DUTERTE ALUMBANA NA BINTI WA CLINTON

0
669

MANILA, PHILIPPINES


RAIS wa Philippine, Rodrigo Duterte amemlaani Chelsea – binti wa Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, wakati akijaribu kutetea ‘utani’ aliofanya kuhusu askari wake kubaka wanawake.

Duterte, rais mtatanishi ambaye amesimamia kampeni ya mauaji ya maelfu ya watumiaji wa mihadarati na ambaye sasa ametangaza amri ya kijeshi akikabiliana na wanamgambo wajiitao Dola la Kiislamu (ISIS), alitumia uhusiano wa kimapenzi wa Clinton na aliyekuwa mfanyakazi wa Ikulu, Monica Lewinsky kumshambulia binti huyo.

Chelsea alikuwa ameungana na wengine wengi mitandaoni kulaani kauli ya Duterte kuwa askari wake wanaweza kubaka hadi askari watatu kila mmoja na kwamba yeye atawajibika kwa hilo baada ya kutangaza amri ya kijeshi katika Jiji la Marawi.

Duterte alisema: “Hawa malaya wamesikia ‘ubakaji’. Kama Chelsea amenishambulia. Sikutania, nilikuwa nikifanya kejeli. Sikiliza hotuba. Huwa sicheki pale ninapofanya utani.

“Nitamwambia wakati baba yako Rais wa Marekani alipokuwa akitembea na Lewinsky na wasichana wengine Ikulu, ulijisikiaje? Je, ulimshambulia baba yako?”

Binti huyo wa Clinton alikuwa ameandika katika mtandao wa tweeter; 'Si utani na haifurahishi kwa kweli.’ Akiitikia kauli za Duterte kuhusu ubakaji.

Aidha aliandika: “Duterte ni muuuaji katili, hajali haki za binadamu. Ni muhimu ifahamike kuwa suala la ubakaji halipaswi kufanyiwa mzaha.”

Askari wa Duterte wanapambana vikali na wapiganaji wa ISIS katika Jiji la Marawi, kusini mwa nchi na kufanya watu 50,000 wakimbie.

Wapiganaji wa ISIS wanaripotiwa kuua watu kwa risasi wanaposhindwa kunukuu Kur’an. 

Muda mfupi baada ya Duterte kutangaza amri ya kijeshi, aliwaambia askari wake: “Kwa sheria hii ya kijeshi na athari na matokeo yake ni mimi pekee nitawajibika.

 “Fanyeni kazi yenu. Mengine niachieni mimi. Nitafungwa jela kwa ajili yenu. Iwapo mtawabaka wanawake watatu, nitasema aliyefanya ni mimi.”

Aidha aliwatuhumu askari wa Marekani kwa kubaka wanawake nchini Philippines na Japan kabla ya kumrudia Clinton.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here