Rais Duterte aliamuru kuuawa kwa wapinzani

0
561
RAIS wa Philippines, Rodrigo Duterte
RAIS wa Philippines, Rodrigo Duterte
RAIS wa Philippines, Rodrigo Duterte

MANILA, PHILIPPINES

RAIS wa Philippines, Rodrigo Duterte, aliamuru kuuawa kwa wanasiasa wa upinzani alipokuwa meya wa zamani wa Davao.

Hayo yamebainishwa na mwanachama mmoja wa kikosi kilichopewa jukumu la kuwaua wafanyabiashara wa mihadarati.

Mwanachama huyo, Edgar Matobato, aliiambia Kamati ya Bunge la Seneti kuwa yeye na wauaji wenzake, waliwaua zaidi ya watu 1,000 katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.

Alielezea kwa kina namna genge hilo lilivyokuwa likitekeleza mauaji hayo ya kutisha dhidi ya washukiwa wa mihadarati, huku akitoa kisa cha kinyama pale wakati walipomgeuza mmoja wa waathirika kuwa kitoweo cha mamba.

Msemaji wa Duterte amepinga madai hayo, huku akisema uchunguzi kuhusu mamlaka ya Duterte akiwa meya, hauendi popote.

Matobato, mwenye umri wa miaka 57, alisema alikuwa mwanachama wa kundi hatari la Davao Death Squad, linalodaiwa kuhusika na mamia ya mauaji.

“Kazi yetu ilikuwa kuwaua wahalifu kama wauzaji dawa za kulevya, wabakaji, wanyang’anyi na kadhalika,” alisema.

Alidai kuwa wapinzani wa kisiasa wa Duterte pia walilengwa, wakiwamo walinzi wanne wa mgombea mmoja wa kiti cha umeya mjini humo, Prospero Nograles.

Waathiriwa walipigwa risasi au kunyongwa, huku baadhi ya wengine wakipasuliwa na kutolewa matumbo na kisha kutupwa baharini ili kuliwa na samaki.

Alikiambia kikao cha Bunge la Seneti, kwamba alitoka katika mpango wa kuwalinda mashahidi na kukimbilia mafichoni, baada ya Duterte kuwa rais, huku akihofia maisha yake.

Aidha Matobato alidai kuwa Duterte aliamuru kulipuliwa kwa msikiti mmoja kulipa kisasi kwa shambulio dhidi ya Kanisa la Davao Cathedral mwaka 1993.

Duterte alikuwa meya wa mji wa Davao mwaka 1988, na msimamo wake mkali ulishuhudia kushuka kwa kiasi kikubwa kwa uhalifu, hatua ambayo ameiendeleza kwenye taifa zima.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here