RAIS BIYA AIONGOZA CAMEROON KUTOKEA NG’AMBO

0
642

YAOUNDE, CAMEROON


RAIS wa Cameroon Paul Biya aliye madarakani kwa miaka 35, amezua hisia kwa kuliongoza taifa hilo muda mwingi kutokea nje.

Akikosolewa na wengi kutokana na staili hiyo ya uongozi, Biya hivi karibuni aliitisha kikao cha Baraza la Mawaziri mara ya kwanza kipindi cha zaidi ya miaka miwili.

Uchaguzi wa urais utafanyika Oktoba mwaka huu, Wacameroon wengi walisubiri kusikia iwapo Biya (85) angetangaza kuwania muhula mwingine.

Lakini hakuna tangazo lililotolewa katika mkutano huo kuhusu hatima ya Biya, aliye madarakani tangu mwaka 1982, akiwa miongoni mwa viongozi wa Afrika walioongoza kwa muda mrefu

Chini yake, Cameroon imenusurika mgogoro wa kiuchumi lakini pia likikumbwa na ufisadi wa kiwango cha juu mbali na kuzorota kwa uhuru wa demokrasia baada ya kufutiliwa mbali kwa ukomo wa urais madarakani mwaka 2008, hatua iliyomfanya awanie tena mwaka 2011.

Safari zake za kigeni zimesababisha makabiliano ya mtandaoni baina ya gazeti la Serikali la Tribune na wanaharakati wa asasi ya kupambana na uhalifu na ufisadi (OCCRP), ambayo ilihesabu muda unaotumiwa naye ugenini kwa kutumia ripoti za magazeti ya kila siku.

Asasi hiyo, ilikadiria kuwa rais alitumia takriban siku 60 nje ya taifa hilo mwaka uliopita kwa ziara za binafsi.

Pia imedaiwa alitumia theluthi moja ya mwaka 2006 na 2009 ughaibuni huku Hoteli ya Intercontinental mjini Geneva, Uswisi ikitajwa kuwa ndiyo anayoipenda zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here