24.1 C
Dar es Salaam
Thursday, October 21, 2021

RAILA: NITAWAADHIBU MAOFISA WA SERIKALI WANAOFANYA SIASA

NAIROBI, KENYA


KIONGOZI mwenza wa muungano wa upinzani wa NASA, Raila Odinga ameonya kuwa akiingia madarakani atawaadhibu vikali mawaziri na makatibu wakuu wanaofanya siasa.

Akiwahutubia wafuasi wa chama chake cha ODM kwenye ukumbi wa Bomas mjini hapa juzi, Odinga aliishutumu Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kwa kuwaruhusu mawaziri na makatibu wa wizara kushiriki siasa.

Alisema kitendo hicho ni kinyume cha Katiba na kwamba chini ya serikali ya NASA maofisa kama hao wataadhibiwa vikali.

 “Serikali ya Jubilee inaendeleza mienendo ya zamani iliyopigwa marufuku na Katiba ya sasa. Rais Kenyatta anapaswa kufahamu kuwa maafisa wa Serikali hawastahili kufanya siasa.”

Awali kiongozi huyo wa upinzani alidai hatua ya Serikali kuruhusu uagizaji mahindi kutoka ng’ambo bila kutozwa ushuru itapelekea kutokea kwa kashfa kubwa serikalini.

Alionya hatua hiyo itatoa mwanya kwa magenge ya mafisadi serikalini, na katika sekta ya kibinafsi kuchuma faida kubwa huku wakulima wa mahindi wakiteseka.

“Ufisadi ni jina jingine la Serikali ya Jubilee. Na mpango wa uagizaji mahindi kutoka ng’ambo bila kutozwa ushuru bila shaka utageuka kashfa nyingine,” alisema wakati wa hafla ya utoaji vyeti vya uteuzi wa moja kwa moja kwa wagombeaji kadhaa wa chama hicho katika ukumbi wa Bomas.

Akisoma bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2017/2018, Waziri wa Fedha Henry Rotich alitangaza kuondoa ushuru unaotozwa mahindi yanayoagizwa kutoka nje, akisema hatua hiyo inalenga kupunguza bei ya unga wa mahindi ambao umepanda mno.

Rotich alisema hatua hiyo inalenga kuwapunguzia wananchi gharama ya maisha.

Awali Jumapili, Waziri wa Kilimo Willy Bett alisema shehena ya kwanza ya mahindi yaliyoagizwa kutoka Mexico itawasili nchini mwishoni mwa mwezi huu.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,644FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles