Raila akana kituo cha matokeo Tanzania

0
684

NAIROBI, KENYA

MGOMBEA urais wa Muungano wa Upizani wa NASA, Raila Odinga, alionekana kukwepa wakati alipoulizwa kuhusu taarifa kuwa upinzani umeanzisha kituo cha kupokea na kuhesabu kura nchini Tanzania.

Awali Odinga alipuuza akisema ni hisia zisizo na ukweli lakini baadaye alisema uwapo wa kituo hicho si kitu kwa vile hakuna sheria inayozuia kuendesha mchakato huo sambamba na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Waziri Mkuu huyo wa zamani alikuwa mshiriki pekee katika mdahalo huo uliofanyika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki (CUEA) mjini hapa kwa wagombea wakuu wa urais, baada ya mpinzani wake Rais Uhuru Kenyatta kukwepa kuhudhuria.

Odinga alizitumia dakika 90 peke yake akieleza ahadi zake za kampeni kama vile kupunguza kodi na kusisitiza kauli zake kuwa vyombo vya usalama vinashirikiana na utawala wa Jubilee kuiba kura katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika siku 13 zijazo.

Odinga alisababisha kicheko wakati alipomwita mtangazaji wa NTV, Linus Kaikai kuwa Joe, akimchanganya na yule wa KTN, Joe Ageyo.

Alipoulizwa kuhusu mpango ulioripotiwa wa kuanzisha kituo cha kupokea na kuhesabu kura nchini Tanzania, ambacho msemaji wa Rais John Magufuli alikana mapema siku hiyo, Raila kwanza alisita na kisha akapuuza taarifa hizo.

“Vitu fulani vinakaa katika hisia za watu. Kwanini tuhitaji kuwa na kituo cha kura nchini Tanzania?” alishangaa.

Alisema kutokana na mahakama kutoa uamuzi kuwa vyama vina haki ya kuhesabu matokeo yao, hakuna haja ya kuhofia.

“Kwanini watu wahofie kituo cha kuhesabu kuwa nchini Ujerumani, Tanzania au hata mwezini? Halipaswi kuwa suala la kuumiza kichwa,” aliongeza.

Wakati alipobanwa kujibu swali moja kwa moja, alisema: “Tuna kituo cha kuhesabu kura nchini Kenya, nchini Kenya na mawinguni”.

Aidha Raila alisema kuwa kuboresha kiwango cha maisha ndiyo itakuwa nguzo kuu ya serikali ya Nasa endapo ataibuka kuwa mshindi.

“Ninawania kiti hiki kwa sababu nimejitolea kuhudumia taifa hili kwa dhati na kulikomboa kutokana na donda ndugu la uongozi mbaya ambao umezidisha umaskini nchini.

“Nitazingatia maisha ya wananchi ikiwemo wanapofanyia kazi na wanapoishi,” akasema kinara huyo wa NASA akieleza jinsi atakavyopunguza na kurahisisha gharama ya maisha ikiwa ni pamoja na vyakula na makazi.

Alisema kuwa serikali yake itabuni muswada utakaodhibiti wenye nyumba kuongeza kodi kiholela na badala yake ipunguzwe ili kila mwananchi amudu maisha.

“Serikali yangu itaweka sheria ambayo mwenye nyumba hataruhusiwa kuzidisha kodi ya kiwango fulani. Wamiliki wa nyumba  wamekuwa wakiongeza kodi kiholela,” alisema akieleza atakavyoitekeleza.

“Asilimia 67 watu wa taifa letu wanaishi mijini. Tutaboresha mashinani kwa viwanda kupitia kugatua sekta mbali mbali na fedha zishamiri ili wananchi waone haja ya kuishi huko badala ya kuhamia mijini,” akaongeza.

Swala la Raila kupunguza kodi ya nyumba limekuwa likiibua mjadala mkali kwa Jubilee ambapo Naibu Rais William Ruto amekuwa akitaka kujua kwa nini kinara huyu apunguze kodi ilhali nyumba hizo si zake.

“Mjadala wa wenye nyumba nimekuwa nikiusikia kwa muda mrefu sana, wajue makazi ndio yake lakini ardhi ni mali ya serikali. Watafute fedha japo wasiwaumize wananchi,” alidokeza Raila.

Kuhusu mada ya ufisadi, Raila alisema chini ya serikali yake, atabuni bodi itakayoangazia ufisadi kwa kina na haitashirikishwa na serikali yake kamwe.

“Bodi hiyo haitahusishwa na serikali hata kidogo. Watumishi wa umma watakaopatikana na sakata za ufisadi watachukuliwa hatua kali kisheria,” alisema akirejelea tume ya inayopambana na ufisadi nchini EACC haijafanya kazi yake ipasavyo.

Alizungumza kuhusu kashfa ya ufisadi  ambapo, Anne Mumbi Waiguru aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi alihusishwa na kupotea kwa sh1.6 bilioni.  Waiguru kwa sasa anawania kiti cha ugavana Kaunti ya Kirinyaga kwa chama cha Jubilee.

“Kwa mfano iwapo ningekuwa serikalini wakati ambapo fedha zilifujwa, washukiwa hao ningewachukulia hatua kali,” alisema.

Kuhus Elimu na ajira kwa vijana, Raila alieleza kuwa serikali yake itayatilia kipaumbele.

“Ajira kwa vijana zimekosekana kwa sababu kila shilingi inayotumika nyingine inaibwa. Hizo fedhan dizo nitatumia kubuni ajira kwa vijana,” alisema.

Afya, usalama, miundo msingi, umoja wa taifa, kupigana na ukabila na kuhusisha walemavu kwenye serikali yake pia yalikuwa ni miongoni mwa maswala aliyosema  serikali yake itayatilia maanani.

Odinga alisema kuwa kwenye siasa, mwanasiasa anapaswa awe na utani anapofanya kampeni na kwamba maneno ya utani ambayo hueleza wapinzani wake yasichukuliwe kuwa kweli.

“Katika siasa unapaswa kuwa na utani, ingawa sikumbuki kumwita Rais Kenyatta mlevi. Huwa simaanishi yeye ni mlevi ninapomtania nikitangaza mpira, wala kuwa Ruto ni mwizi.

“Rais husema mimi ni ‘Mundu Muguruki’ (mwendawazimu), Ruto husema mimi ni mtu wa vitendawili, wote huwa hawamaanishi hivyo na pia huwa simaanishi hivyo. Huo ni utani tu,” alisema akifanya watu waangue kicheko.

Kinara huyu alisema endapo uchaguzi mkuu utakuwa wa huru, haki na uwazi, akibwagwa atakubali.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here