24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Raia wa Cameroon, Nigeria wadakwa Pwani wakiwa na karatasi za kuchapisha fedha

Na Gustafu Haule, Pwani

WATU wawili raia kutoka nchi za Afrika Magharibi wamekamatwa mkoani Pwani kwa tuhuma za kuishi nchini kinyume cha sheria, ambapo katika upekuzi mmoja alikutwa akiwa na karatasi zilizoandaliwa kwa ajili ya kuchapisha noti za fedha.

Raia hao waliokamatwa ni Livingson Ese Onayomake kutoka Nigeria na Bertrand Noubissie kutoka Cameroon ambao wote walikutwa katika eneo la Mapinga Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani katika nyumba ya New Era Nyembe anayedaiwa alikuwa mke wa Betrand.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari leo Februari 14, 2023 Mjini Kibaha, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema raia hao wamekamatwa baada ya taarifa kutoka kwa raia wema waliokuwa na hofu kuhusiana na uraia wao pamoja na shughuli wanazofanya.

Kunenge amesema Februari 10, mwaka huu timu ya maofisa Uhamiaji walifika katika eneo la tukio na kufanya upekuzi ambapo waliwakuta raia hao wawili kila mmoja akiwa hana hadhi ya kiuhamiaji.

Amesema katika upekuzi huo Betrand amekutwa na karatasi zilizoandaliwa kwa ajili ya kuchapisha noti za pesa, kemikali na kasia (safe) la kutunzia fedha.

Aidha raia huyo wa Cameroon amekutwa  na pasipoti  namba 0441270 iliyotolewa Yaounde Cameroon Aprili 12, 2016 ambayo iliisha muda wake Aprili 12, 2021 na aliingia nchini Novemba 2, 2019 na viza aliyopewa iliisha muda wake Februari 1, 2020.

Naye, Livingson Ese Onayomake raia wa Nigeria alikutwa na pasipoti 34 ambazo si za kwake, ambapo kati ya hizo 32 ni za Nigeria na mbili ni za Ghana ambazo alidai alizichukua  kwa lengo la kuwatafutia Viza Uturuki.

Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Pwani, Omary Hassan.

Livingson anadaiwa kuingia nchini Februari 11, 2020 na kupewa viza ya matembezi ya siku 90 ambayo iliisha Mei 10, 2020 ambapo anadaiwa kuendelea kuishi nchini kinyume cha sheria hadi alipokamatwa .

Mtuhumiwa huyo raia wa Nigeria hakukutwa na Pasipoti alipoulizwa alieleza kuwa aliiweka rehani kwa Dayana wa hoteli ya King Sinza  Afrika sana  ili aweze kumpa fedha ya kujikimu.

Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Pwani, Omary Hassan amesema Februari 9, walipokea taarifa kutoka kwa msiri kwamba katika eneo la Mapinga,kuna watu ambao uraia na mienendo yao inatia mashaka ambapo, Februari 10, mwaka huu timu ya Maafisa Uhamiaji walifanikiwa kufika katika eneo husika na kutekeleza jukumu lao  na kuwakamata watuhumiwa hao.

Imeelezwa kuwa uchunguzi dhidi ya watuhumiwa hao umekamilika kwa hatua stahiki kuchukuliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles