29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Raia 1800 wa Burundi waomba hifadhi nchini

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

RAIA wa Burundi waliongia nchini na kuomba hifadhi wamefikia 1,852 hadi sasa.

Taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga, ilieleza raia hao waliingia nchini kupitia vijiji mbalimbali vya Mkoa wa Kigoma.

Alivitaja vijiji hivyo kuwa ni pamoja na Kigaye, Sekeoya na Kakonko. Vingine ni Kosovo, Kagunga na Kibuye, huku wengine wakiwa wamepitia katika Kituo cha Uhamiaji cha Manyovu kilichopo mkoani humo.

Alisema baada ya kufanyiwa mahojiano ya kina katika kituo maalumu kilichopo mjini Kigoma, raia 1,252 kati yao wamehamishiwa katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu iliyoko wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

“Mahojiano yanaendelea kwa waliobaki na wanaoendelea kuwasili. Shughuli ya kuwahoji na kuwahamishia katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu inafanywa na Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi (UNHCR), pamoja na wadau wengine,” alisema Nantanga.

Alisema Serikali za vijiji zinasaidia kuwapokea na baada ya kufanyiwa ukaguzi, hatimaye wanasafirishwa hadi mjini Kigoma.

Msemaji huyo alisema licha ya ujio wa raia hao, hali ya ulinzi na usalama katika maeneo wanapoingilia ni shwari na hadi sasa hakuna matukio yoyote ya uhalifu yalitolewa taarifa.

Alitoa wito kwa raia wanaoishi katika maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Burundi mkoani Kigoma kutoa taarifa kwa Serikali za vijiji vyao kuhusu wageni wanaofika katika maeneo yao, badala ya kuwahifadhi kiholela majumbani mwao, na kwamba watakaobainika kukiuka maagizo hayo watachukuliwa hatua za kisheria.

Alisema raia hao ambao wamekuwa wakiingia nchini wakiwa katika vikundi vidogo vidogo wataendelea kupokelewa kufuatana na taratibu na sheria zinazotawala upokeaji wa waomba hifadhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles