31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

RAHA, KARAHA ZA KUFIKA KILELENI MLIMA KILIMANJARO

 

Wahabari, maofisa wa TANAPA wakiwa kileleni Mlima Kilimanjaro.

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA

HAIKUWA rahisi kufika katika kilele cha Mlima Kilimanjaro, mita 5,895 kutoka usawa wa bahari. Nilitamani kuishia katikati ya Uhuru Peak na Stella Hut mita 5,756.

Mlima huo mrefu kuliko yote iliyosimama duniani, unaopandika bila vifaa mahsusi, unapatikana kilomita 330 Kusini mwa Ikweta, ukiwa na theluji ya kudumu jambo ambalo limekuwa likishangaza wapanda milima.

Ulitangazwa kuwa Hifadhi ya Taifa mwaka 1973 na kufunguliwa kwa utalii mwaka 1977. Mwaka 1987 UNESCO ililitangaza kuwa eneo la urithi wa dunia na 2013 ilitangazwa moja ya maajabu saba ya Afrika.

Safari ilianza Desemba 4, mwaka jana ikuhusisha wanahabari 15, maofisa wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Brigedia Jeneral Jairo Mwaiseba na Kiongozi wa msafara Jeneral Mstaafu na Mwenyekiti wa Bodi ya TANAPA George Waitara.

Wengine ni Balozi Charles Sanga na wanadiplomasia. Lengo likiwa ni kuadhimisha Siku ya Uhuru Desemba 9, mwaka huu na kuhamasisha utalii wa ndani.

Desemba 4, mwaka huu, kundi la wanahabari wakiwa ofisi za Kampuni ya Utalii ya Zara Tours mjini Moshi, walianza kujionea maajabu ya nguo na vitu vinavyohitajika kwa mtu anayekwenda kupanda mlima.

Baada ya kukabidhiwa vifaa timu ilirejea kulala kwa safari Desemba 5, mwaka jana. Saa mbili asubuhi safari ilianza kwa mbwembwe na bashasha kutoka kwa kila mtu.

Getini Marangu, timu ya wanahabari iliungana na askari  na maofisa wa JWTZ wakiongozwa na Jenerali Mstaafu Waitara ambaye amekuwa akipanda Mlima Kilimanjaro kila Desemba 9.

Marangu ndipo ilipo njia kuu ya kupandia hapo kulifanyika hafla ya kuwaaga na Waziri wa Maliasili na Utalii, Professa Jumanne Maghembe aliwakabidhi bendera ya Taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TANAPA, Jeneral Mstaafu Waitara pamoja na mambo mengine alionya wanaojishughulisha na ujangiri akisisitiza siku zao zinahesabika.

Aliiambia timu ya watu 36; “Tutatambuana mbele ye safari.” Baada ya hapo safari ilianza chini ya kiongozi mkuu (Chief Guide) Faustine Chombo kutoka Kampuni ya Utalii ya Zara Tours.

Safari iligawanyika katika makundi matano ya kilomita nane kutoka Marangu mpaka Mandara chenye mita 2,720.

Hapo kuna baadhi walianza kulalamikia matumbo ya kuharisha, vichwa kuuma huku wakitapika kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Safari ya mlimani huhusisha uoto wa ukanda wenye mkusanyiko wa kipekee wa kanda tofauti za Ikolojia, hali ya hewa yenye kukuonyesha safari fupi iliyopo sawa na kutoka Ikweta hadi Aktiki.

Kuanzia getini Marangu mwinuko wa mita 1800 -2800 mpaka kituo cha Mandara huwa ni yenye uoto wa asili na msitu wa milima. Baada ya kuwasili wageni walipewa nyumba za kulala, zilizojengwa kwa mbao.

Pamoja na baridi katika safari hiyo, bado wageni hutakiwa kunywa maji takribani lita tatu mpaka nne kwa siku ili kuzuia maumivu ya kichwa na mwili kuchoka.

Asubuhi siku iliyofuata safari ya Horombo kilomita tisa ilianza kwa kila mtu kubeba begi (Day Park), ambalo huwa na vitu vinavyoweza kuhitajika wakati wowote, kwani begi kubwa huwa limetangulia mbele na wapagazi.

Eneo hili la mwinuko wa mita 1800-4000 lina maua, magugu na nyasi, lilivutia zaidi machoni. Haikuwa rahisi kuitafuta Horombo kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa ya upepo, jua wakati mwingine ukungu.

Ukiwa hapo usiku mji wa Moshi na maeneo ya jirani, ukiwamo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), huonekana vizuri na kufanya uvutike kukaa nje.Ni baridi tu ndio itakayokuingiza ndani.

Siku ya tatu wapanda mlima hulazimika kupumzika ili  kuzoea hali ya hewa, ambapo hutembelea eneo la Zebra linalovutia likipambwa na kilele cha Mawezi. Lakini pia miamba yenye rangi nyeupe na nyeusi.

Saa 11 jioni, siku hiyo nje kulisikika nyimbo zilizosababisha wageni kutoka kuona kinachoendelea. Looh, kumbe ni burudani iliyoongozwa na (Guide Rasta) aliyekuwa akiwaimbisha Wajapani.

Wimbo huo wa “Oooh Chura anaruka bila boxer, ukimuona anainama, anainuka, anaona hayaa huyooo,” uliwafanya wageni wengi kujiunga na kuimba ili tu kutafuta joto mwilini.

Siku ya nne safari ilihusisha kilometa tisa za kutembea eneo la mwinuko wa mita 4000-5000, uoto wa jangwa la milimani na mimea iliyotawanyika, inayobadilika kutokana na hali tofauti ya mwinuko.

Saa 9 alasiri tuliwasili Kibo Hut mita 4,720 huku baadhi wakionyesha dalili za kutoendelea na safari ya kileleni saa nne usiku, chai iliandaliwa kisha chakula na kutakiwa kulala mpaka saa nne usiku tayari kwa safari ya kilomita sita hadi kufika kileleni.

Mwandishi Angelo Mwoleka wa Star Tv, hakutaka kabisa kuamshwa akidai kujiskia ovyo. Wakati Theodora alikuwa akitokwa machozi na kila alichokiona kilikuwa kibaya kwake.

Saa 4:30 usiku wapanda mlima walivaa nguo nzito na kupanga mstari kila mmoja akiwa na tochi mbele ya taji la uso, begi na fimbo.

Safari ilianza kwa hatua fupi usiku huo, mwendo wa zigizaga ili kuukata mwinuko mkali, huku maneno ya hamasa kama “Kili Team, huuhaaa,” yakitawala waongoza watalii.

Tangu safari kuanza mwandishi Deo Kassami alionyesha kushindwa akidai mama alimwambia; “Ukiona mtu hatoi hewa chafu (kujamba), hapumui vizuri, basi yupo mbioni kufa.” Hivyo aliamua kurejea chini.

Kibo Hut mpaka Gilman’s pana mabadiliko ya hali ya hewa, mawe na kukabiliwa na usingizi, kuishiwa nguvu, kutapika na matumbo kuvuruga.

Siku ya tano asubuhi tuliwasili Gilman’s mita 5,685 tukiongozwa na Brigedia Jeneral Mwaseba.

Ukanda wa kileleni una jotoridi chini ya sentigredi sifuri, ukipambwa na majabali ya theluji. Kituo cha Stella kundi jingine lilirudi, huku Uwesu akidai amekanyaga barafu na Siwayombe akidai aende Uhuru Peak kufanya nini?

Hatimaye wanahari na vyombo wanavyoandikia kwenye mabano; Eliya Mbonea (Mtanzania), Charles Ndagula, Dickson Busagaga (Tanzania Daima), Zulfa Mussa (Mwananchi), Ramadhani Mvungi (Star Tv), Paschal Shelutete (TANAPA) na wanajeshi walifika kileleni.

Kileleni kuna maajabu yake kwani majabali ya barafu huonekana mithili ya maghala ya kuhifadhia chakula.

Safari ya kurejea ilianza siku hiyo mpaka Horombo, timu ililala kisha siku ya sita ilishuka Marangu na kupokelewa kwa shangwe na nderemo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles