22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

PWANI INAHITAJI MBINU HIZI KUKABILIANA NA MLOLONGO WA MAUAJI

TULIANDIKA, tukaandika na sasa tunaandika tena juu ya mlolongo wa mauaji ya kutisha yanayofanywa katika Mkoa wa Pwani, hasa katika wilaya zake za Kibiti na Rufiji na watu ambao vyombo vya ulinzi ama havijawatambua au havijaamua kuwaweka wazi.

Habari hizi zinatisha na kushangaza na zinaibua maswali lukuki, ikizingatiwa kuwa, kundi kubwa la watu wanaouawa ni maaskari na viongozi wa vijiji na kata wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tulipata kuandika huko nyuma kwamba si vizuri sana yanapotokea matukio kama haya kuanzisha mjadala wa kuumiza, lakini ni vizuri kuanzisha mjadala wa kuhoji na hata kuchimbua  kinachosababisha matukio yenyewe na ikiwezekana kubuni hatua ambazo Jeshi la Polisi linaweza kuzichukua ili kuepuka changamoto ya namna hii mbele ya safari.

Kuna maswali mengi ambayo pengine si tu Jeshi la Polisi, bali na watu wa kada mbalimbali wanajiuliza kwa lengo la kupata sababu ni kwanini matukio haya yamekuwa yakijirudia rudia tena ndani ya muda mfupi. Ni maswali magumu, lakini yanahitaji kupatiwa majibu.

Matukio haya yote yanatokea katika wakati ambao Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama tunaona vimechukua hatua fulani Fulani, ikiwamo kuanzisha ngome katika maeneo korofi.

Mazingira ya matukio yote ambayo tumesikia yakifanywa katika maeneo hayo, yanatoa picha halisi ya aina ya watu wanaotekeleza.

Utafiti unaohusu mambo ya uhalifu uliofanywa na wataalamu wa saikolojia mwanzoni mwa mwaka 2000 katika magereza mbalimbali ndani na nje ya nchi ya Marekani, ulibaini kuwa watu wenye kiwango kidogo cha elimu, tena wasio na utaalamu wengi wao walithibitika kufanya uhalifu kama ule wa ukabaji, wizi wa kuvunja nyumba, ofisi na maeneo mengine, wizi wa magari na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Lakini katika utafiti huo huo, ukaonyesha kuwa watu hao wenye kiwango kidogo cha elimu kwa kawaida ni nadra kuhusika kwenye matukio makubwa, tena wakiwa mstari wa mbele kama kuvamia maeneo hatari, yakiwamo yale yanayohusu jeshi.

Hivyo kwa vyovyote, ukiyatazama matukio ya mauaji yanayofanywa katika maeneo ya Mkoa wa Pwani na mengine yaliyopita, unaweza kusema kwa uhakika kwamba yametekelezwa na watu wenye utaalamu uliochochea ujasiri wa kufanya vitendo hivyo vya kinyama vya kuua binadamu wenzao.

Pia baadhi ya Polisi na wataalamu wengine wa sheria wanalifahamu hili la sababu zinazosababisha watu wafanye uhalifu, zipo nyingi, kuna sababu za kibaolojia, kiuchumi, kisaikolojia na zile zinazotokana na jamii na ndiyo maana tunaona kuna wale wanaofanya uhalifu ili wapate mali, fedha na chochote.

Lakini wapo wanaofanya uhalifu kwa sababu ya hasira, kulipa kisasi, wivu na wengine ni kwa sababu ya ujivuni wao.

Pamoja na hayo, wataalamu wa masuala ya uhalifu, wanasema wanaofanya uhalifu kwa nia ya kujipatia chochote kama mali au fedha hawa mara nyingi wanafanya ukabaji, wanavunja kama nyumba au mahali popote, ikitokea mara chache sana wanaua lakini ni nadra sana.

Kwa upande wa wale wanaofanya uhalifu kama njia ya kutaka kudhibiti, kulipa kisasi au kupata nguvu ya kuongoza, hawa mara nyingi wanatajwa kufanya uhalifu ule wa kuua, kuumiza au kubaka. Na wanasema matukio haya yanatokea wakati ule ule ambapo kiwango cha hasira kinakuwa juu, au kuna hisia fulani fulani mbaya.

Kwa sababu hiyo, tunadhani huenda mlolongo wa matukio ya mauaji katika Mkoa wa Pwani ukawa umeangukia kwenye kundi hilo la aina ya uhalifu.

Pamoja na yote, uchunguzi ni muhimu kuona kama lipo kundi ambalo limelipa kisasi, au limeamua kudhibiti kwa sababu fulani fulani.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles