Putin, Xi Jinping wamfunika Trump kuaminiwa duniani

0
791

WASHINGTON, MAREKANI

Utafiti mpya umeonesha watu wengi duniani wanamwamini zaidi Rais wa Urusi, Vladimir Putin, kuliko mwenzake wa Marekani, Donald Trump.

Kwa mujibu wa utafiti ambao umetolewa juzi na Kituo cha Utafiti cha Pew Research Centre chenye makao yake makuu mjini hapa, kati ya watu 26,112 waliohojiwa kutoka mataifa 25, asilimia 30 wanaamini Rais Putin anafanya vitu sahihi duniani, asilimia 34 wakimwamini Rais wa China, Xi Jinping wakati asilimia 27 ndio walisema Rais  Trump ameanzisha sera mbadala katika masuala ya uhusiano kimataifa.

Watafiti hao walisema Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amezidi kupanda chati kwa kuaminiwa baada ya kujikusanyia asilimia 52, akifuatiwa na Kiongozi wa Ufaransa, Emmanuel Macron mwenye asilimia 46.

Utafiti huo pia umeonesha kwamba idadi kubwa ya umma inaelezea wasiwasi mkubwa juu ya jukumu la Marekani katika kushughulikia masuala ya kimataifa.

“Idadi kubwa ya waliohojiwa walisema Marekani haijali masilahi ya nchi nyingine wakati wa kufanya uamuzi kuhusu sera za nje.

“Wengi wanaamini Marekani inafanya kwa kiwango cha chini ili kusaidia kutatua changamoto kubwa duniani kuliko ilivyokuwa mwanzo,” ulieleza utafiti huo uliozinduliwa juzi.

Ulieleza pia kwamba jukumu la China katika masuala ya kiuchumi duniani limeongezeka zaidi  katika kipindi cha miaka 10 ingawa kwa kiasi kikubwa watu wamekuwa wakiamini Marekani ndilo taifa linaloongoza kiuchumi duniani.

Pia kwa upande wa raia wa Urusi ambao walikuwa wakimwani Rais Trump, utafiti unaonesha kuwa wamepungua kutoka asilimia 53 hadi 19 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here