27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Putin kumzidi maarifa Trump?

NA MARKUS MPANGALA

WIKI hii kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un na Rais wa Urusi, Vladimir Putin wamekutana mjini Vladivostok, Mashariki mwa Nchi ya Urusi. Mkutano huo ni wa kwanza kati ya viongozi hao wawili, wamejadiliana umuhimu wa kuimarisha uhusiano wao kisiasa na kidiplomasia kwa malengo ya kupata suluhisho la suala la silaha za nyukilia kwenye rasi ya Korea. 

Aidha, viongozi hao wamejadili kudhoofika kwa uhusiano wa biashara kati ya nchi zao kwa asilimia 56 mwaka 2018 kutokana na vikwazo vilivyowekewa na Serikali ya Korea Kaskazini.

Nchi zote mbili yaani Urusi na Korea Kaskazini zinakabiliwa na vikwazo kutoka sehemu zinazofanana. Kwa msingi huo Urusi na Korea Kaskazini hazina chaguo jingine zaidi ya kuimarisha ushirikiano, huku zikitegemea zaidi mshikamano wao na Nchi ya China ambayo imekuwa ikihusiana nazo vizuri kidiplomasia, kiuchumi, ulinzi na usalama. 

Msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov ameviambia vyombo vya habari kuwa mkutano baina ya viongozi hao umepangwa kwa minajili ya kubadilisha hali ya hewa ya uhusiano wao,  huku mataifa yote yakikabiliwa na vikwazo. Korea Kaskazini imewekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa, mataifa ya Ulaya na Marekani. Wakati Urusi imewekewa vikwazo na Marekani pamoja na mataifa ya Ulaya. 

Korea Kaskazini inawahitaji washirika wapya na wa zamani ili kuendeleza mshikamano katika kipindi ambacho imewekewa vikwazo. Urusi nayo inahitaji washirika ambao itakuwa nao bega kwa bega katika kujenga uchumi wa nchi yake pamoja na kuongeza ushawishi miongoni mwa mataifa.

Urusi imependekeza kuwa Korea Kaskazini na Marekani zinapaswa kurudi kwenye meza ya mazungumzo ili kuhakikisha suala lenye mgogoro mkubwa duniani yaani silaha za nyukilia linapatiwa ufumbuzi. 

Korea Kaskazini nayo imekuwa ikitoa masharti yake ili kuhakikisha inatii masharti yanayotolewa na mataifa ya ulaya, Marekani na Umoja wa Mataifa kama njia ya kukomesha majaribio ya silaha za nyukilia. 

Sharti la Marekani na ambalo limechangia vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini, ni kwamba lazima Serikali ya Kim Jong Un iachane kabisa na mpango wa kutengeneza silaha za Nyukilia. 

Sharti hili limekuwa gumu kwa Korea Kaskazini kwani inahitaji kufanya biashara na mataifa ya kigeni pamoja na kuhakikisha vikwazo dhidi yake vinaondolewa. 

Tangu Rais Donald Trump achukue madaraka nchini Marekani alianza kuwa na mvutano mkubwa na kurushiana maneno huku Kim Jong Un naye akiendeleza majaribio ya silaha za nyukilia na kukiuka ilani ya kimataifa. Hatua hiyo ilikuwa tishio kwa jirani zake Japan na Korea Kusini. 

Trump aliapa kupambana ikiwa Kim Jong Un iwapo nchi yake itaendelea kutishia kuirushia makombora ya masafa marefu Marekani, wote wakipeana majina ya kukebehi.

Korea Kaskazini ilikaidi na kufanya jaribio la nyukilia la sita mwezi Septemba mwaka 2017. Baadaye Kim alitangaza kuwa nchi yake imefanikiwa mpango wake wa kua taifa la nyukilia, ikiwa na silaha zinazoweza kuifikia ardhi ya Marekani.

Kim Jong Un na Trump wamekutana mara mbili katika mikutano yenye nia ya kuondokana na msuguano pamoja na vikwazo vilivyopo baina ya mataifa hayo. Mkutano wa kwanza ulifanyika nchini Singapore Juni mwaka jana, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Marekani viongozi hao wawili walikutana kwanza kwa dakika 41 na walikuwa wawili na wakalimani wao wakati wakijadiliana juu ya makubaliano waliyopaswa kufanyika kwa masilahi ya nchi zote mbili.

Mkutano wa mjini Hanoi nchini Vietnam, hakukuwa na makubaliano yoyote kwani kila upande ulishikilia msimamo wake. Korea Kaskazini iliambiwa iache matumizi na urutubishaji wa silaha za nyukilia kama sharti la kufikia mwafaka wa mgogoro baina yake na mataifa makubwa. 

Kwa upande wake Kim Jong Un alisisitiza kuwa ili atekeleze masharti aliyopewa ni muhimu kwa Umoja wa Mataifa kuondoa vikwazo vyote dhidi ya Korea Kaskazini ambavyo vinahusiana na mipango ya kutengeneza silaha eneo la Yongbyon.

Hoja ya pili iliyosababisha Marekani ione kikao hicho hakikuwa na manufaa hivyo kuondoka mezani ni msimamo wa Korea kaskazini kuwa ipo tayari kuondoa vinu vya Yongbyon pekee na si vinu vyote vya nyukilia vya Korea Kaskazini. Marekani imekataa matakwa ya Korea Kaskazini ya kutaka kuondolewa kwa vikwazo vyote.

Mwaka 2011 Urusi ilishirikishwa katika mazungumza ya mpango wa nyukilia wa Korea Kaskazini. Kiongozi wa zamani wa taifa hilo Kim Jong-il, alikutana na rais wa Urusi wa wakati huo Dmitry Medvedev.

Korea Kaskazini imekuwa ikiendelea na shughuli zake za nyukilia. Mapema Aprili mwaka huu taifa hilo lilidai kuwa limefanyia majaribio silaha yake mpya, ambayo duru za kisiasa inadhani ni kombora la masafa mafupi.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Dmitry Peskov, mazungumzo ya mgogoro katika rasi ya Korea yalianza rasmi mwaka 2002, ambapo yalihusisha Korea kaskazini, Korea kusini, China, Japan, Urusi na Marekani.

“Hakuna mpangilio rasmi wa mazungumzo hadi kipindi hiki. Lakini kwa upande mwingine, hatua zilizofikiwa zimefanywa na nchi nyingine. Manufaa yaliyopo ni kuungwa mkono kutatua mgogoro, lengo likiwa ni kusitisha michakato yote ya utengenezaji wa silaha za nyukilia, na kuhakikisha msuguano baina ya nchi mbili za Korea unamalizika,” alisema Peskov alipozungumza na vyombo vya habari.

Mkutano wa Kim Jong Un na Vladimir Putin umetafsiriwa kuwa ni fursa kwa Korea Kaskazini kuonyesha nguvu zake pamoja na kuwa na nchi zinazounga mkono juhudi zake kwenye mazungumzo yake ya Marekani. 

Korea Kaskazini imemlaumu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, kutokana na kuvunjika mazungumzo ya Februari mwaka huu mjini Hanoi. Pia imependekeza waziri huyo aondolewe kwenye kamati ya majadiliano kuhusu nyukilia kwa madai anaongeza mambo mengi ya kipuuzi. Vilevile imependekeza kuteuliwa mtu makini na mwangalifu kwenye mazungumzo yao.

Mkutano huo pia ni fursa kwa Korea Kaskazini katika kutengeneza mwelekeo wa uchumi wake bila kutegemea Marekani. Kim Jong Un ameripotiwa kumwambia Putin juu ya umuhimu wa kuondolewa vikwazo dhidi ya nchi yake.

Wachambuzi wa masuala ya kidiplomasia wanasema mkutano huo pia ni fursa kwa Urusi kuonyesha umuhimu na ushawishi wake katika utatuzi wa mgogoro wa rasi ya Korea. Urusi kama zilivyo Marekani na China hazina furaha kutokana na mgogoro unaoendelea kati ya Korea kusini na Korea kaskazini. 

Katika kipindi cha vita baridi, Muungano wa Sovieti (Urusi ya sasa) ilikuwa rafiki mkubwa wa Korea Kaskazini ambapo ilitoa misaada ya kijeshi pamoja na kushirikiana kibiashara. Korea Kaskazini inafuata itikadi ya kikomunisti kama ilivyokuwa Urusi, wakati Korea Kusini inafuata itikadi ya kibepari inayopo Marekani na washirika wake. Kufuata itikadi zinazofanana kulitengeneza urafiki mkubwa baina ya mataifa hayo.

Baada ya kuvunjika muungano wa Sovieti mwaka 1991, biashara kati ya mataifa hayo ilidorora ambapo Korea Kaskazini iliamua kuelekeza nguvu zake katika uhusiano wake na China, ambayo ni rafiki mwaminifu hadi sasa.

Chini ya uongozi wa Rais Putin, Urusi ilijikwamua kiuchumi na mwaka 2014 alifuta madeni yote ya nchi yake kwa Korea Kaskazini ikiwa ni ishara ya kuanza upya uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo.

Duru  za kisiasa zinasema, je ni kwa kiasi gani Urusi itafanikiwa kuwashawishi Korea Kaskazini ambayo wamefanya mkutano mmoja, kuliko Marekani iliyofanya mikutano miwili bila kupatikana mwafaka?

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles