Moscow, Urusi
Rais wa Urusi, Vladimir Putin amesema hataki kulirejesha Taifa hilo kwenye enzi ya Kisovieti ya watawala kufia mamlakani bila ya kuwaandaa warithi wao.
Kauli ya Putin imekuja katika wakati ambapo minong’ono inaongezeka kuhusu mustakabali wake kufuatia mabadiliko makubwa ya kisiasa aliyoanzisha wiki iliyomalizika jana.
Putin aliyeko mamlakani kwa miongo miwili alisema hayo baada ya kuulizwa iwapo anafikiria kuondoa vifungu vya kikatiba vinavyohusu ukomo wa urais wakati alipokutana na maveterani wa Vita vya pili vya dunia katika mji wa Saint Petesburg juzi.
Putin anayetarajiwa kuachia ngazi mwaka 2024 alisema anaelewa kile alichokiita wasiwasi wa watu kuhusu kuendelea kuwepo madarakani huku akisema mipango ya mpito ya Taifa hilo ulikuwa muhimu siku chache baada ya mapendekezo ya kushtukiza ya mabadiliko makubwa ya kikatiba yaliyosababisha serikali kujiuzulu na uteuzi wa waziri mkuu mpya.