Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Profesa Bonaventure Rutinwa amewahimiza Watanzania kujifunza lugha ya Kichina na kupata ujuzi juu ya utamaduni na mila zake.

Amesema tayari Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza Kichina kuwa miongoni mwa lugha za kigeni kufundishwa katika shule za msingi na sekondari hivyo, ni wajibu wa Watanzania kuchangamkia fursa hiyo.
Profesa Rutinwa ametoa wito huo Januari 25,2025 wakati wa sherehe za Mwaka wa Mpya wa Jadi wa China wa Nyoka ambao ndiyo tamasha kongwe na muhimu zaidi la kitamaduni nchini China linalosherehekewa na familia zote.
“Tukio hili litaleta matokeo chanya kwa Tanzania na China, naamini litawahimiza wanafunzi na wageni wetu kujifunza lugha ya Kichina na kupata ujuzi juu ya utamaduni na mila zake.
“Wale wanaositasita lini watanza wanapaswa kusoma Kichina kuanzia sasa na kuendelea,” amesema Profesa Rutinwa.
Aidha amepongeza mafanikio ya Taasisi ya Confucius (CI) ya Udsm na kusema ni taasisi muhimu katika kubadilishana utamaduni na kujifunza lugha ya Kichina pamoja na kukuza uelewa wa pamoja wa ushirikiano wa kirafiki kati ya China na Tanzania.
Profesa Rutinwa amewashukuru wadau wa taasisi hiyo yaani Kampuni ya Ujenzi na Mawasiliano ya China (CCCC), Group Six na wengine kwa kutoa fursa za ajira kwa wanafunzi wa shahada na diploma.

“Makampuni mengi zaidi ya China yanahimizwa kuwekeza na kuendeleza biashara nchini Tanzania. Wanahitaji wakalimani, mafundi na wafanyakazi wengi wenye asili ya Kichina. Wanakuja Cl au kuwasiliana na wakurugenzi wakiomba wahitimu wafanye nao kazi,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa CI – Udsm, Profesa Zhang Xiaozhen, amesema kutokana na kuongezeka kwa makampuni ya Kichina nchini, idadi ya wanafunzi wanaosoma Kichina pia inaongezeka.
“Tutajitahidi kutoa mafunzo kwa walimu wa Kichina katika shule za msingi na sekondari ili kuwezesha shule nyingi za msingi na sekondari kutoa kozi za Kichina,” amesema Profesa Zhang.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Taasisi ya kuendeleza urafiki kati ya Tanzania na China, Joseph Kahama, amesema urafiki wa China una manufaa makubwa kwani kila mwaka nchi hiyo imekuwa ikitoa ufadhili wa Watanzania kwenda kusoma, kujifunza mambo mbalimbali na kutalii.

Amesema mwaka jana walikwenda Watanzania 200 na mwaka huu Serikali ya China itatoa ufadhili wa watu 450.
Sherehe hizo zilizoandaliwa na CI na CCCC Tawi la Tanzania, yalijumuisha burudani mbalimbali kutoka kwa wanafunzi wa Udsm na vyuo vingine wanaojifunza lugha ya Kichina na kula pamoja vyakula mbalimbali vya Kichina.