24.8 C
Dar es Salaam
Thursday, September 21, 2023

Contact us: [email protected]

PROFESA NDULU AWAPIKU VIGOGO SERIKALI YA MAGUFULI

magu

Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM,

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, amejitofautisha na vigogo wengine ndani ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, ikiwamo kutoa ushauri kwa kiongozi huyo wa nchi kwa mujibu wa taaluma yake na eneo ambalo analiongoza.

Katika kipindi cha miezi 12 ya utawala wake, Rais Magufuli amewatikisa watumishi wa umma, huku baadhi ya vigogo wakishindwa kutoa kauli yoyote kwa hofu ya kutumbuliwa.

Hadi sasa, tayari vigogo zaidi ya 300 wameshatumbuliwa na kiongozi huyo wa nchi pamoja na mawaziri husika kutokana na makosa mbalimbali, ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka na ufisadi.

Msimamo wa Gavana Ndulu kwa Rais Magufuli, ulianza kuonekana Machi 10, mwaka huu siku ambayo kiongozi huyo wa nchi alifanya ziara ya kushtukiza BoT na kumwagiza kusitisha malipo ya malimbikizo ya madeni (Ex-Checker) ya Serikali yanayofikia Sh bilioni 925 na badala yake yarejeshwe Wizara ya Fedha na Mipango kufanyiwa uhakiki.

Sambamba na agizo hilo, pia alimtaka Gavana Ndulu kupitia upya orodha ya wafanyakazi wa BoT na kuwaondoa wale wote ambao hawana ulazima wa kuwapo katika ajira.

“Haiwezekani tukawa na kundi kubwa la wafanyakazi, wanalipwa mishahara wakati hata kazi wanazofanya hazijulikani.

“Maswali ninayoyauliza ni ‘very technical’, yapo mengine siwezi kuyataja hapa ‘and I know what iam doing’. Muyafute majina yote ya watu ambao si wafanyakazi wa BoT ili mshahara uende kwa watu wanaofanya kazi hapa,” alinukuliwa Rais Magufuli.

Ziara hiyo ilikuwa ya pili tangu Dk. Magufuli alipoapishwa kuwa rais Novemba mwaka jana. Alitembelea ofisi hizo akitokea Ikulu kwa miguu na kubaini kuwapo utoro ofisini kwa baadhi ya wafanyakazi wa Hazina.

Hata hivyo, wakati Rais akitoa maagizo hayo, BoT ilikuwa na wafanyakazi 1,391 katika matawi yake sita yaliyopo nchi nzima, huku taarifa kutoka ndani ya taasisi hiyo zikisema kulikuwa na upungufu wa wafanyakazi katika Idara ya Utafiti.

Siku moja baada ya Rais Magufuli kueleza kutoridhishwa na mwenendo wa ajira za watumishi wa BoT na ulipaji wa malimbikizo ya madeni ya Serikali, Gavana Ndulu alitoa kauli inayojibu hoja hizo.

Kuhusu kuhakikiwa upya kwa malipo ya malimbikizo ya madeni ya Serikali yaliyotajwa na Rais Magufuli, alisema siyo hundi bali ni mapendekezo ya wizara na idara mbalimbali za Serikali yanayopitishwa katika bajeti kwa matumizi.

“Hakuna fedha zilizorudi Hazina, tatizo watu wanaongea vitu ambavyo hawavijui, hivi ‘exchequer’ mnajua maana yake ni nini? Mnaandika cheque (hundi).

“Zile ni ‘exchequer’, haya ni mapendekezo ambayo wizara na taasisi mbalimbali wanapewa mamlaka ya kutumia. Hutolewa baada ya bajeti na zinapotolewa ile ni ruhusa ya kutumia na si kulipa, unalipa kama zipo fedha, sisi hatuna na kama hamna fedha huwezi kulipa,” alisema Gavana Ndulu.

Alifafanua kuwa taasisi hiyo ambayo ni mhimili mkuu wa uchumi wa Taifa, hutoa malipo ya mapendekezo endapo wizara zinazoomba malipo hayo zina fedha katika akaunti zao na si vinginevyo.

Akijibu hoja ya kuwapo kwa watumishi hewa BoT, alisema hana watumishi wa aina hiyo.

“Hilo jambo ni la kuniuliza mimi au yeye? (Rais Magufuli), nilisema nitalifanyia kazi na kuhakiki hicho kilichosemwa, yeye amepata taarifa, tutalifanyia kazi, ‘unless’ (labda) kama mna ‘information’ (taarifa) mnaweza kutupa,” alisema.

Aidha kuvunjwa kwa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kauli ya Rais Magufuli juu ya sababu za kuvunjwa kwake, ni mtihani mwingine ambao Gavana Ndulu aliweza kusimamia kile alichokiamini kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa sheria, Gavana wa BoT ni mjumbe wa Bodi ya TRA yenye jumla ya watu tisa ambao watano wanaingia kwa mujibu wa sheria na wanne ni wa kuteuliwa.

Siku chache baada ya kuivunja Bodi ya TRA, Rais Magufuli alisikika akisema kuwa aligundua bodi hiyo imeshirikiana na menejimenti kuweka mabilioni ya fedha katika akaunti maalumu (fixed deposit account) katika benki za biashara kwa lengo la kuzihujumu.

Akihutubia mahafali ya Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) wilayani Kibaha mkoani Pwani, Rais Magufuli alisema: “Juzi hapa tumekuta Sh bilioni 26 zilizokuwa zimetolewa TRA kwa ajili ya matumizi ya TRA, zikapelekwa kwenye mabenki matatu kama ‘fixed deposit account’ na bodi ikapitisha.

“Ndiyo maana nilipozipata hizo hela; hela nikazichukua na bodi kwaheri,” alisema Rais Magufuli alipokuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 31 ya chuo hicho yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani.

Akijibu mojawapo ya maswali ya waandishi wa habari mjini Arusha siku chache baada ya kauli hiyo ya Rais Magufuli, Gavana Ndulu aliweka wazi kwamba TRA kuweka fedha katika akaunti maalumu katika benki za biashara si kosa kisheria.

Profesa Ndulu ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Bodi ya TRA iliyovunjwa na Rais Magufuli, alisema kuwa hakuna hasara kiuchumi kuweka fedha katika akaunti hizo, isipokuwa suala hilo lilikuwa na hali nyingine.

Japokuwa Profesa Ndulu hakutaka kufafanua zaidi kwa maelezo kwamba alichomekewa na waandishi wakati akielezea hali ya uchumi, alisema hali hiyo ndiyo suala lililozungumzwa na siyo kusema “fixed deposit account” ni mbaya.

Profesa Ndulu alisema hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua athari za kiuchumi kwa taasisi za umma kuweka fedha katika akaunti maalumu, tena benki binafsi.

“Kwani amesema fixed account zote ni mbaya? Pamoja na za watu binafsi? Ndiyo hivyo sasa. Nilijua mtachomekea hilo kwa hiyo nilikuwa tayari,” alisema mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles