33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

PROFESA NDULU ATWAA TUZO YA GAVANA BORA AFRIKA

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


GAVANA mstaafu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, ametunukiwa tuzo ya mwaka 2018 ya gavana bora barani Afrika na jarida maarufu la African Banker.

Sherehe za kutoa tuzo hizo zilifanyika jijini Busan, Korea Kusini juzi jioni katika mikutano ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inayoendelea kuanzia Mei 21 hadi 25 mwaka huu.

“Tuzo hii nimepewa kutokana na mchango mkubwa kutoka BoT wakati wa uongozi wangu. Kwa hiyo tuzo hii ni heshima kubwa kwangu na kwa Benki Kuu ya Tanzania.

“Awali niliwaomba waandaaji nao walikubali kwamba Dk. Namajeje Weggoro, Mkurugenzi Mtendaji wa AfDB, Kanda ya Afrika Mashariki, apokee tuzo hiyo kwa niaba yangu.

“Sikujua kama Naibu Gavana wa BoT, Julian Banzi Raphael, anashiriki katika mikutano ya AfDB vinginevyo yeye ndiye angepokea kwa niaba yangu,” alisema Profesa Ndulu katika taarifa iliyotolewa na BoT jana.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa jarida la African Banker, Omar Ben Yedder, Prof. Ndulu ametunukiwa tuzo hiyo kutokana na mchango wake mkubwa katika kukuza huduma jumuishi za kifedha na kuchangia katika kuhakikisha zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanafikiwa na huduma rasmi za kibenki.

“Wewe (Profesa Ndulu) ni mwanzilishi barani Afrika na duniani kote. Umekuwa mstari wa mbele hasa katika kuandaa kanuni na usimamizi makini wa sekta ya kibenki pamoja na kuhamasisha usahihi na utendaji bora katika sekta hiyo,” alisema Yedder katika barua yake ya mwaliko kwa Profesa Ndulu.

Hii ni mara ya tatu kwa Profesa Ndulu kushinda tuzo ya Gavana Bora wa Benki Kuu barani Afrika.

Mwaka 2009 alitangazwa kuwa Gavana Bora wa mwaka kwa Afrika na Jarida la Emerging Markets linalochapishwa jijini London, Uingereza.

Sherehe hizo zilifanyika katika mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) iliyofanyika Istanbul, Uturuki.

Aidha, Profesa Ndulu alishinda tuzo ya pili ya Gavana Bora wa Benki Kuu barani Afrika mwaka 2015 iliyotolewa na jarida lingine maarufu la Africa Investor jijini New York wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Alitunukiwa tuzo hizo kutokana na mchango wake mkubwa katika kufanikisha upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha kwa wananchi walio wengi pamoja na kuvutia na kuandaa mazingira bora ya uwekezaji barani Afrika.

Profesa Ndulu amekuwa Gavana wa BoT kwa muda wa miaka 10 tangu mwaka 2008 hadi mwaka 2018.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles