29.3 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

Profesa Ndalichako: Tutahakikisha vyuo vya kimkakati vinatoa mafunzo yenye weledi

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema mipango ya Serikali ni kuhakikisha vyuo vya kimkakati kikiwemo Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kinatoa mafunzo kwa weledi wa hali ya juu na kwa kutumia vifaa vya kisasa.

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Profesa Zacharia Mganilwa, akimuonyesha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako moja ya vifaa vitakavyotumika kufundishia kozi ya uhandisi wa matengenezo ya ndege.

Akizungumza wakati wa kupokea vifaa vya kufundishia wahandisi wa matengenezo ya ndege vilivyotolewa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), amesema serikali imejipanga kuhakikisha inaweka nguvu kwenye maeneo ya kimkakati ili kuwa na wataalam wa kutosha.

“Serikali imekuwa ikisisitiza mafunzo yanayojenga ujuzi, mafunzo kwa vitendo na imekuwa ikihimiza vyuo vyetu vikuu vihakikishe kwamba wanafunzi wanafanya mafunzo zaidi na kuanzisha programu nyingine ambazo zinalenga katika kuwajengea wanafunzi ujuzi wenye viwango vya kimataifa,” amesema Profesa Ndalichako.

Amesema vifaa hivyo vitakiongezea chuo uwezo wa kutoa elimu bora zaidi kwenye usafiri wa anga na kuwa na mafunzo yanayoakisi na yanayolenga kutatua changamoto mbalimbali za jamii.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Bahati Gruzye, amesema vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 245 vimetolewa kwa ajili ya Shule Kuu ya Anga NIT kupitia ruzuku inayotolewa na Mfuko wa Elimu baada ya chuo hicho kuwasilisha maombi.

“Ruzuku iliyotolewa kwa NIT ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la msingi la Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na TEA. Kupitia mfuko huu ufadhili kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya elimu na ununuzi wa vifaa hutolewa katika ngazi zote za elimu kwa Tanzania Bara na elimu ya juu kwa Tanzania Zanzibar,” amesema Gruzye.

Amesema lengo ni kuongeza jitihada za serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia sambamba na kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha NIT, Profesa Zacharia Mganilwa, amesema wahitimu watakaotumia vifaa hivyo watakuwa mahiri na soko la ajira litafaidi.

“Hatuna shaka walimu wa kozi hii ya matengenezo ya ndege watavitumia vifaa hivi kuwafundisha wanafunzi vizuri kwa vitendo. Vina mazoezi mengi sana mwalimu anaweza akatengeneza tatizo kwenye mfumo wa ndege halafu wanafunzi wakalitatua, kwahiyo pindi watakapohitimu watakuwa na umahiri zaidi na naamini soko la ajira litafaidi sana wahitimu watakaotumia hivi vifaa,” amesema Profesa Mganilwa.

Amevitaja vifaa vilivyopokelewa kuwa kile kinachofundisha mfumo wa bawa la ndege na mfumo wa tairi la ndege, kinachomfundisha mwanafunzi namna mifumo ya injini inavyofanya kazi, vifaa vinavyoendeshwa kwa mfumo wa upepo kuwawezesha wanafunzi waweze kujua namna hewa inavyotengenezwa na inavyosaidia katika matumizi mbalimbali ya ndege.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,225FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles