23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

PROFESA MAJI MAREFU KUAGWA LEO DAR

Na WAANDISHI WETU – DAR/TANGA


MWILI wa Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (CCM), unatarajiwa kuagwa leo katika viwanja vya Karimjee Dar es Salaam na mazishi kufanyika kesho mkoani Tanga.

Mbunge huyo maarufu kama Profesa Maji Marefu, alifariki dunia juzi saa 3:20 usiku katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam alikolazwa kwa matibabu.

Kaka wa marehemu, Hilary Ngonyani, jana aliliambia MTANZANIA kuwa mwili huo unatarajiwa kuagwa kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana kisha kusafirishwa kwenda Korogwe mkoani Tanga kwa mazishi.

“Hapa tupo kwenye maandalizi ya safari ya kesho baada ya kuagwa na wabunge wenzake na wananchi wa Jiji la Dar es Salaam, tutasafiri hadi Korogwe ambako Alhamisi wananchi na ndugu watauaga na kisha mazishi yatafanyika,” alisema Ngonyani.

Alisema Profesa Maji Marefu alilazwa Muhimbili kwa siku 10 kabla ya kufikwa na umauti, akisumbuliwa na homa ya baridi yabisi (Animonia), kichefu chefu kilichoambatana na kuumwa tumbo pamoja na kichwa.

“Marehemu amekuwa na historia ya kuugua mara kadhaa miaka ya nyuma, kidogo aliugua akapelekwa India kutibiwa kwa tatizo la miguu, lakini kipindi hiki ameugua na kulazwa Muhimbili kwa siku 10,” alisema.

Ngonyani alisema kifo cha mdogo wake kimeacha pengo katika familia kwa sababu walikuwa wanashauriana katika masuala mbalimbali.

“Tulikuwa tunaendana, sasa najihisi kupungukiwa, ni jambo kubwa, sasa sina mkubwa mwenzangu, nimeachwa na watoto wadogo watupu, nimekuwa mkiwa,” alisema Ngonyani.

TAARIFA YA BUNGE

Katika hatua nyingine, Bunge limesema baada ya kikao cha Kamati ya Uongozi na familia ya marehemu, wamekubaliana kuwa mazishi yatafanyika kesho katika makaburi ya Kwa Mndolwa kwa kutanguliwa na ibada itakayofanyika nyumbani kwa marehemu wilayani Korogwe.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa Bunge kwa kushirikiana na familia, linaendelea kuratibu taratibu za mazishi ya mbunge huyo na taratibu zaidi zitaendelea kutolewa.

TAARIFA YA CCM

CCM kupitia taarifa yake iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Hamphrey Polepole, ilileza kupokea kwa mshtuko na huzuni msiba wa Profesa Maji Marefu.

“Wakati wote wa uongozi wake alikuwa sehemu ya viongozi wa kisiasa, ambao waliamini katika uelewa wa pamoja wa matarajio ya kisiasa ya Watanzania, ujenzi wa siasa safi na za kimaendeleo, alipenda kusimamia haki, uongozi bora na umuhimu wa kuweka nchi na taifa mbele.

“Uongozi wa CCM, chini ya Mwenyekiti Dk. John Magufuli na Katibu Mkuu Bashiru Ally, unapenda kutoa salamu za pole kwa familia ya marehemu, ndugu jamaa, marafiki, wanachama wa CCM hasa kutoka Mkoa wa Tanga, wapigakura wa Jimbo la Korogwe Vijijini na wote walioguswa na msiba huu,” ilieleza taarifa hiyo ya chama.

ALILIWA

Mbunge wa Tanga, Alhaji Mussa Mbaruku (CUF), alisema wamepokea msiba huo kwa mshtuko mkubwa kutokana na ukaribu uliokuwapo baina ya Profesa Maji Marefu na wabunge wengine wa mkoa huo.

“Kwa kweli familia imepata pigo kubwa, kwani hazijapita hata siku 20 mkewe alipofariki na jana (juzi) amefariki baba yao hivyo niwape pole, nimwombe Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira kwenye kipindi hiki kigumu, lakini niwape pole wabunge wa CCM kwa kuondokewa na mwenzao,” alisema.

Mbaruku alisema mbunge huyo alikuwa na ushirikiano mkubwa na wabunge wengine wa Mkoa wa Tanga jambo ambalo lilimjengea heshima kubwa kwa jamii.

Alisema hatasahau namna alivyokuwa akipigania jimbo katika masuala mbalimbali ya maendeleo kama vile barabara.

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alimwelezea marehemu kama mtu aliyekuwa na upendo na ushirikiano kwa watu wote bila kubagua.

“Kwa kweli msiba huu ni mkubwa sana kutokana na upendo aliokuwa nao kwa wananchi wake, hivyo tumwombee kwa mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi,” alisema Waziri Ummy.

Mbunge wa Lushoto, Shabani Shekilindi alimaarufu Bosnia (CCM), alisema msiba wa Profesa Maji Marefu ni pigo kwa wakazi wa Korogwe na mkoa mzima wa Tanga kutokana na mapenzi na ucheshi wake kwa watu wote.

Alisema kupitia mbunge huyo, wabunge wapya wa mkoa huo waliochaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, walijifunza mambo mengi kutoka kwake na kwamba alikuwa mwalimu kwake.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya CCM, Dk. Edmund Mndolwa, aliitaka familia kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Aliwataka wananchi kuendeleza yale mema aliyokuwa akiyafanya Profesa Maji Marefu kutokana na kuwatumikia vema watu wa Korogwe enzi za uhai wake.

MSIMAMO WAKE BUNGENI

Profesa Maji Marefu ambaye wakati wa uhai wake alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili Tanzania, atakumbukwa kwa misimamo yake kuhusu tiba asili na waganga wa kienyeji.

Miongoni mwa michango yake inayokumbukwa zaidi, ni pale alipowaonya wabunge wanaojifananisha na waganga wa kienyeji pale wanapotaka kuchangia jambo fulani.

Alionya hayo wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha 2016/17, alipowashangaa wabunge wanaowabeza waganga wa kienyeji wakati siku za nyuma waliwategemea kutokana na kutokuwa na hospitali katika maeneo yao.

“Sasa leo hii kila atakayefanya makosa hapa anafananishwa na mganga wa kienyeji, jana kuna mtu hapa kachangia anasema askari wakikosa kazi watakwenda kuwa waganga wa kienyeji, hii ni biashara gani mnafanya hapa, hiki ndicho kilichowaleta hapa?” alihoji Profesa Maji Marefu.

Katika hoja yake hiyo, aliwataka wabunge kutowaona waganga wa kienyeji kuwa ni watu dhaifu kwa kuwatolea mifano mibaya ilihali wakati wa uchaguzi ndio wateja wao wakuu.

“Naomba kuanzia leo mkichangia changieni hoja, msiwafananishe watu wakati usiku mko majumbani kwao mnakwenda kutibiwa. Badala ya kusema hospitali zenu hazina dawa, nyie mnaona fahari kutaja waganga wa kienyeji,” alisema Profesa Maji Marefu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles