24.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

PROFESA LIPUMBA: MAALIM SEIF ANAIDHOOFISHA CUF


 Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM   | 

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahimu Lipumba amemtupia lawama Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa ndiye anakidhoofisha chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana wakati akisoma maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama hicho, alisema Maalim Seif amekidhoofisha chama hicho kwa kutotekeleza azimio la baraza hilo lililomtaka kufungua kesi Mahakama Kuu ya Zanzibar kupinga kufutwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Kesi hizo zingefunguliwa CUF ingekuwa na wawakilishi 27  wa majimbo na viti maalum, idadi ya  wawakilishi wa kuchaguliwa  na viti maalum wa CUF ingekuwa sawa na idadi ya wawakilishi wa CCM na hivyo  Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar ingekuwa na mawaziri wa CUF,’’ alisema Prof Lipumba.

Alisema kutokana na Maalim Seif kushindwa kufanya hivyo kumesababisha CCM kubaki peke yao  ndani ya baraza na kutunga sheria watakavyo wao ikiwa ni pamoja na kubadilisha sheria ya uchaguzi.

“Pamoja na mazingira haya magumu, Baraza Kuu limeagiza  juhudi kubwa zifanyike kulinda katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 inayotaka  kuwapo kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa.

“Pia linamshauri Rais Dk. John Magufuli kwa nafasi yake kujiwekea ajenda ya kuimarisha  demokrasia nchini ikiwa ni pamoja na kulinda haki za binadamu, kuheshimu haki za vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara na uhuru wa vyombo vya habari nchini kufanya  kazi zao kwa mujibu wa sheria ,’’ alisema Lipumba.

HALI YA UCHUMI

Profesa Lipumba alisema Baraza linatambua na kupongeza jitihada za serikali katika ukusanyaji wa mapato na kutekeleza miradi  mikubwa ikiwemo  kujenga reli ya kisasa, kufua umeme  wa maji  kwenye maporomoko  ya Mto Rufiji na kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda.

Baraza Kuu hilo limeelezea chaguzi ndogo za marudio ya serikali kwamba limesikitishwa kwa kuvunjwa utaratibu  za uchaguzi katika chaguzi ndogo za marudio na kuitaka Tume  kujirekebisha na kuhakikisha wasimamizi wake wanafuata sheria.

“Ni aibu kwa Tanzania kuwa na chaguzi zisizokuwa huru na za haki, miaka 27  baada ya mfumo wavyama vingi kuanzishwa, hivyo kuitaka tume hiyo kujitathmini na kujipanga upya,’’ alisema Lipumba.

UCHAGUZI WA MITAA

Alisema Baraza Kuu limepitisha mapendekezo  ya mkakati wa chama ya kujiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu wa 2020 na kuagiza kamati ya utendaji iandae program ya utekelezaji huo.

Pia limeagiza ajenda na Ilani ya CUF itaongozwa  na itikadi ya chama ya haki sawa kwa wote, ambazo ni pamoja na haki za kiuchumi, kijamii, kisiasa na za mazingira safi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles