PROFESA KITILA AIPA MTIHANI DAWASA

0
630

NA TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM


KATIBU Mkuu wa Wizara Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo, ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam(DAWASA) kuharakisha uchimbaji wa visima vya maji vya Kimbiji na Mpera ili kuwaondolea adha inayowakabili wakazi wa jiji hilo na Mkuranga mkoani Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya ziara katika mradi huo juzi Profesa Mkumbo alisema kukamilika kwa visima hivyo kutaongeza wingi wa maji katika eneo la huduma ya Dawasa kutoka lita milioni 300 mpaka 720.

Alisema  maji hayo yataweza kutoshereza mahitaji kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam na mkoa wa Pwani hadi mwaka 2032.

“Mradi unaendelea vizuri na nimeridhika na jitihada zinazofanywa na Dawasa pamoja na wakandarasi kwani tayari visima 17 kati ya 20 vimekamilika na viko katika hatua ya upimaji wa maji hivyo ni vema waongeze kasi kuukamilisha,” alisema Prof. Mkumbo.

Alisema mradi huo unatekelezwa na serikali ya Tanzania kupitia wakandarasi NSPT kutoka nchini Iran na Serengeti ya Tanzania kwa gharama ya dola milioni 18.3 sawa na Sh bilioni 40.

“Kila kisima kinatarajiwa kuzalisha jumla ya lita milioni 260 na hivyo kukamilika kutakuwa neema kwa wakazi wa Kigamboni, Mji mpya Kongowe, Gongolamboto, Pugu, Chanika, Mbagala na mji wa Mkuranga mkoani Pwani pamoja na baadhi ya vitongoji vyake,” alisema Profesa Mkumbo.

Hivi karibuni Rais Dk. John Magufuli, alizindua miradi ya upanuzi wa mtambo wa Ruvu juu na ulazaji wa mabomba na kuridhishwa na kazi iliyofanywa na Dawasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here