24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

PROFESA KABUDI ATANGAZA MABADILIKO MFUMO MAWAKILI

Mwandishi wetu


WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema kuanzia sasa mawakili walioko kwenye ofisi ya Mwanasheria Mkuu na wanasheria wote katika Wizara, Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi za Serikali watakuwa ni Mawakili wa Serikali.

Alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dodoma jana.

“Kwa miaka mingi kumekuwa na ombwe la usimamizi wa wanasheria walio kwenye utumishi wa umma. maamuzi mengi yamekuwa yakifanyika pasipo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuwa na taarifa. Mambo yanapoharibika ndio Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inataarifiwa ili kuokoa jahazi,” alisema.

Alisema hali hiyo kwa miaka mingi imekuwa ikiisababishia Serikali kuingia kwenye migogoro na kuingia hasara.

“Baada ya mabadiliko haya, wanasheria wote walioajiriwa katika utumishi wa umma wanakuwa wanafanya kazi na kutumia mamlaka ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndani ya wizara zao, taasisi zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa,” alisema.

“Vilevile wanasheria hao watakuwa chini ya uangalizi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Nia ya mabadiliko haya ni kumuwezesha Mwanasheria Mkuu wa Serikali awe na usimamizi juu yao na kuwazuia kufanya kazi bila kufuata maelekezo yake.”

Prof. Kabudi alisema mashirika yote ya kimkakati kama vile Bandari, Tanesco nayo pia yataletwa chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuepuka kuitia Serikali hasara.

“Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye mashirika haya, lakini kuna maamuzi yanafanyika wakati Ofisi ya Mwanasheria Mkuu haina taarifa,” amesema.

“Kutokana na  marekebisho hayo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaratibu na kusimamia mawakili wa Serikali walio katika ofisi hiyo na wanasheria wote katika wizara, Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi za Serikali ambao sasa watakuwa ni mawakili wa Serikali.

Aidha, mawakili wa Serikali walio katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali watakuwa chini ya uratibu na usimamizi wa Mkurugenzi wa Mashtaka na Wakili Mkuu wa Serikali,” amesema.

Alisema marekebisho hayo yanakusudia kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa mashtaka ya jinai nchini hususani utekelezaji wa azma ya Serikali ya kutenganisha shughuli za upelelezi na uendeshaji wa mashtaka.

“Kuanzishwa kwa ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kunalenga kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa mashauri ya madai na kuiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuimarika katika weledi na ubobezi wa kitaalamu katika kuishauri Serikali na kuandika miswada ya sheria kwa kuzingatia mabadiliko makubwa katika tasnia ya sheria kitaifa, kikanda na kimataifa,” ameongeza.

Hata hivyo, Prof. Kabudi alisema mabadiliko yoyote hayawezi kuleta matokeo yaliyokusudiwa kama watendaji hawatabadili mtizamo wao. Ni kweli muundo uliobadilishwa ulikaa kwa miaka mingi na inawezekana mambo mengi yalikuwa yanafanyika kwa mazoea.

“Kutokana na mabadiliko haya, tunakiri kuwa mitizamo yetu na ya watumishi wenzetu lazima ibadilike. tumejipanga kuhakikisha kuwa watumishi hawafanyi kazi kwa mazoea ili wasiwe na tashwishwi wala ajizi katika kutekeleza majukumu ya umma,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles