25.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 31, 2023

Contact us: [email protected]

Profesa Kabudi asema serikali itatengeneza fursa

MWANDISHI WETU- DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Mambo ya Nje Na Ushiriano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema serikali ya awamu ya tano itaendelea kutengeneza fursa nyingi za ajira ili kuwezesha wahitimu wengi wa vyuo vikuu kupata ajira na kutumia utaalamu walioupata kujenga taifa lao.

Hayo aliyasema jana wakati akizungumza kwenye mahafali ya kwanza ya kwa wanafunzi waliosoma nje ya nchi kupitia Kampuni ya Global Education Link, yaliyofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Waziri Kabudi alisema serikali inaendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi katika kuweka mazingira mazuri, yatakayoongeza fursa nyingi za ajira kwa vijana wanaomaliza vyuo vya nje na ndani ya nchi.

Aliwapongeza wahitimu hao kwa kwenda kusoma nje ya nchi na kurudi na ujuzi, ambao watautumia kujenga taifa lao katika sekta mbalimbali kama ujenzi wa miundombinu na zingine zilizopo.

“Serikali ya awamu ya tano inaendelea kutekeleza awamu ya pili ya mpango wa maendeleo kwa ufanisi mkubwa sana, pia inataka kujenga uchumi wa kati ambao utaongeza nafasi nyingi za ajira kwa vijana wetu,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema serikali imejipanga kuendelea kudhibiti mianya ya ufisadi ili fedha zinazopatikana zielekezwe katika miradi ya maendeleo kupunguza umaskini kwa watanzania wa mijini na vijijini.

Waziri aliipongeza Global Link Education kwa namna ambavyo imeweza kuwapeleka zaidi ya wanafunzi 5,600 kwenda kusoma vyuo vikuu nje ya nchi na kufuatilia maendeleo yao hadi walipohitimu masomo yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Global Link Education, Abdulmalik Mollel alisema mahafali hayo ni ya kwanza kufanyika hapa nchini na kwamba mwaka huu pekee kampuni hiyo inatarajia kupeleka wanafunzi 1,000 kusoma nje ya nchi.

Alisema mamia ya wanafunzi ambao walipelekwa nje kusoma, wengine wamepata bahati ya kuwa wakurugenzi wa makampuni na wengine wamejiajiri na wengine wameajiriwa kwenye taasisi mbalimbali hapa nchini.s

Mollel alisema baadhi ya wahitimu hao bado wanatafuta fursa, hivyo aliwaomba wawekezaji nchini kuhakikisha wanawapa kipaumbele vijana hao katika nafasi za ajira badala ya kuajiri wataalamu kutoka nje.

“Tuna vijana wenye ujuzi wa kutosha katika taaluma mbalimbali, mheshimiwa Waziri nakuomba hili ulibebe utusaidie, ili zinapotokea nafasi za ajira vijana wetu wapate nafasi kwasababu ujuzi wa kutosha wanao,” alisema.

“Hawa vijana wamesoma kwao wanajua tamaduni zao wanajua kila kitu kuhusu nchi zao, kwa hiyo mimi naona huu ni muda mwafaka kwa wawekezaji wanaokuja nchini watoe kipaumbele kwa vijana hawa wapate ajira,” alisema Mollel.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,315FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles